RAIS John Magufuli ametoa agizo la maji yaliyokuwa yametoka siku moja
kabla ya kufika Kata ya Tinde katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
yasiwe nguvu ya soda ya kutoka siku hiyo kwa kumuona yeye na baada ya
hapo kutoendelea na kuwafanya wananchi kuendelea kuteseka.
Hayo aliyasema jana baada ya Diwani wa kata hiyo, Jafari Kanoro
kupewa ruhusa ya kusalimia wananchi wake na kumueleza Rais kuwa
changamoto kubwa iliyokuwepo ni uhaba wa maji ambapo jana yake yalianza
kutoka rasmi baadhi ya maeneo baada ya kazi iliyofanywa usiku na mchana
na mafundi.
Ilielezwa mkutanoni hapo kuwa, maji hayo yametoka baada ya miaka mitatu ya mateso ya kukosa maji safi na salama.
Rais Magufuli alisema kilio cha wananchi hao amekisikia, hivyo kama
maji hayo yametoka kwa siku hiyo yasiwe nguvu ya soda, bali yawe
endelevu kwa siku zote ikiwa bado kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa
Victoria utakaopita Tinde na kuelekea mkoani Tabora.
“Mimi ndugu zangu nasema kuwa mradi wa maji tayari tumepewa kiasi cha
shilingi milioni 600 na Serikali ya China, hivyo fedha hizo
tutazisambaza kwenye mikoa mbalimbali yenye uhitaji wa mradi wa maji
ambapo hata hapa Tinde nitawahurumia kuwatengea fungu hilo,” alisema
Rais Magufuli.
Aliwaambia wananchi wa eneo la Isaka na Kagongwa kuwa changamoto ya
uhaba wa maji ataitatua, hivyo wamuunge mkono na kumuombea ili atimize
ahadi zake alizokuwa akiziahidi kipindi cha uchaguzi.
Pia alisema kitendo cha wanawake kuchota maji umbali mrefu
kinamsikitisha ikiwa hali hiyo nayo imeonekana kuchangiwa kwa maambukizi
ya virusi vya ukimwi (vvu) kwa baadhi yao kufanyiwa vitendo vya ukatili
hasa kubakwa wakati wa kutafuta maji.
Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum alisema ameshukuru Serikali ya
Awamu ya Tano kumpatia mradi wa maji ambao umeanzia Kata ya Tinde
ukitarajiwa kunufaisha vijiji 30.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment