NDEGE za kijeshi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zitaruka
angani kesho Septemba Mosi, kuadhimisha miaka 52 ya kuanzishwa kwa jeshi
hilo.
Taarifa hiyo ilitolewa na Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali Ngemela
Rubinga, alipokuwa akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, ratiba ya maadhimisho ya siku hiyo mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kanali Rubinga, ndege hizo zitarushwa kwa ajili ya kutoa heshima kwa Watanzania ambao ndio waajiri wa JWTZ.
“Miaka 52 ni mingi na tunajivunia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kulinda amani katika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Kwa hiyo, siku hiyo ndege zitaruka kuwaonyesha wananchi jinsi jeshi lao lilivyo pamoja nao.
“Pamoja na kurusha ndege hizo, siku hiyo pia tutaiadhimisha kwa
kufanya usafi katika maeneo mbalimbali kama sehemu ya kuiunga mkono
Serikali ya awamu ya tano ambayo imekuwa ikisisitiza kufanya usafi.
“Pia, siku hiyo tutachangia damu katika hospitali mbalimbali na
madaktari wetu watakuwa wakitoa ushauri kwa wagonjwa kuhusiana na
magonjwa mbalimbali.
“Kwa wale wasiofahamu, maadhimisho haya yalianza kuadhimishwa wiki
moja iliyopita, lakini Septemba mosi ndiyo kilele chake ambapo shughuli
nyingi zitafanywa ikiwa ni pamoja na magwaride yatakayofanyika katika
kambi zetu kama sehemu ya kukumbushana masuala mbalimbali,” alisema.
Naye Makonda alipokuwa akipokea ratiba hiyo, alisema wananchi
wasiogope pindi watakaposikia milio ya ndege za kijeshi bali
wazishangilie ndege zao kwani siku hiyo ni ya amani.
“Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka na tunaamini wananchi wanajua
hivyo, kwani ni sherehe muhimu na kuna kila sababu ya kujivunia jeshi
letu la JWTZ kwa mafanikio waliyoyapata kwa miaka 52.
“Katika utekelezaji wa jambo hilo, wakuu wa wilaya hapa Dar es Salaam
wameshajipanga kwa ajili ya kujumuika na jeshi kufanya usafi na kama
kuna wananchi au taasisi zozote zitakazotaka kuunga mkono kufanya usafi
siku hiyo, zifike ofisini kwangu ili wapangiwe maeneo,” alisema Makonda.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment