Utafiti
mpya umebaini kupungua pakubwa kwa idadi ya samaki katika Ziwa
Tanganyika, mojawapo ya maziwa muhimu zaidi kwa uvuvi duniani,
kumetokana na ongezeko la joto duniani katika karne moja iliyopita.
Ziwa Tanganyika ndilo la kale zaidi Afrika na samaki wake huwa muhimu sana kwa lishe katika mataifa yanayopakana na ziwa hilo.
Lakini idadi ya samaki imepungua sana, huku wavuvi wakiendelea kuongezeka.
Ongezeko hili la wavuvi lilidhaniwa kuwa chanzo kikubwa cha kupungua kwa idadi ya samaki.
Lakini utafiti mpya unaonesha chanzo hasa ni ongezeko la joto duniani kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ziwa
Tanyanyika ndilo la pili kwa ukubwa duniani miongoni mwa maziwa yenye
maji yasiyo na chumvi na maji yake huwa katika mataifa manne: Burundi,
Jamhuri ya KIdemokrasia ya Congo, Tanzania na Zambia.
Samaki kutoka kwa ziwa hilo hutoa asilimia 60 ya protini zitokanazo na wanyama ambazo huliwa na watu eneo hilo.
Aidha, ni eneo lenye aina nyingi ya wanyama na mimea.
Ili kufahamu mabadiliko yanayotokea katika ziwa hilo, watafiti wamechukua sampuli za mchanga kutoka kwenye kina cha ziwa hilo.
Baada
ya kufanya utathmini wa mchanga huo na visukuku, wamepata viashiria
kwamba idadi ya samaki imekuwa ikishuka sambamba na ongezeko la joto
duniani.
Wanasayansi wanasema katika maziwa yanayopatikana maeneo
yenye joto karibu na ikweta, ongezeko la joto katika maji hupunguza
kuchanganyikana kwa maji kutoka sehemu ya juu ya ziwa ambayo huwa na
oksijeni pamoja na maji yenye virutubisho vingi sehemu ya chini kwenye
ziwa.
Kutochanganyikana vyema kwa maji haya husababisha virutubisho
vinavyofika juu kwenye ziwa kupungua, hili hupunguza ukuaji wa miani
(mimea ya rangi ya kijani, kahawia au nyekundu inayoota chini ya bahari)
na hili hupelekea kupungua kwa lishe ya samaki.
Watafiti waliohusika
katika utafiti huo wanasema ongezeko la joto limepunguza
kuchanganyikana kwa maji, kupungua kwa ukuaji wa miani pamoja na
kupungua kwa maeneo ambayo viumbe waishio chini ya bahari wanaweza
kuishi na kustawi.
"Wazo letu lilikuwa kuchunguza visukuku na kubaini
kushuka kwa idadi ya samaki kulianza wakati gani," anasema Prof Andrew
Cohen kutoka Chuo Kikuu cha Arizona.
"Iwapo hili lilifanyika kabla ya
kuanza kwa uvuvi wa kiviwanda miaka ya 1950, basi ungekuwa na ushahidi
mkubwa kwamba hili halitokani na ongezeko la uvuvi na hivi ndivyo
tulivyobaini."
Wanasayansi hao hata hivyo hawajapuuzilia mbali athari za ongezeko la uvuvi katika miongo sita iliyopita.
Wanasema
kumekuwa an ongezeko la watu tangu miaka ya 1990, hasa kutokana na
wakimbizi waliotoroka mizozo na kuhamia maeneo yaliyo karibu na ziwa
hilo.
"Ukizingatia mtindo wa sasa wa kuendelea kugawika zaidi kwa
maji kwenye ziwa, idadi ya samaki itaendelea kupungua. Watu wanaosimamia
sera wanafaa kuanza kufikiria kuhusu chanzo mbadala cha mapato na lishe
kwa watu wanaoishi eneo hilo."
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kisayansi la Proceedings of the National Academy of Sciences.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment