GAZETI hili jana lilichapisha habari yenye kichwa cha habari ‘Kiama cha wauza ‘unga’ chawadia.’
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba katika mpaka wa Tunduma mkoani Songwe, ndiyo iliyoibua habari hiyo.
Katika ziara hiyo, Waziri alitoa siku 14 kwa maofisa wanaohusika na
udhibiti wa dawa za kulevya mpakani hapo, kuwakamata watu wanaohusika na
uvushaji wa dawa hizo kutoka nchini kwenda nchi jirani ya Zambia na
nyingine zilizopo ukanda huu.
Bila kupoteza maneno, Waziri Nchemba alisema Tanzania hivi sasa
imechafuka kutokana na wimbi la usafirishaji wa dawa za kulevya na kutoa
mifano kwamba nchini China kuna Watanzania zaidi ya 200 wanashikiliwa
kwa tuhuma za dawa za kulevya na kutaja nchi nyingine zenye wahalifu
kutoka Tanzania kuhusiana na dawa za kulevya ni pamoja na Pakistan,
India na Afrika Kusini.
Sisi tunaunga mkono agizo la Waziri la kuwasaka na kuwatia mbaroni
wahalifu hao wa dawa za kulevya ili wakabiliane na mkono wa sheria na
kupata wanachostahili kwa uhalifu huo.
Taarifa kwamba sasa Tanzania imefikia hatua kwa baadhi ya nchi
kufikiria kuongeza masharti zaidi kwa kila atakayejitambulisha nje ya
nchi kuwa ni Mtanzania, yanatuweka katika hali siyo nzuri miongoni mwa
macho ya mataifa mengine duniani.
Mtazamo huo wa nchi nyingine dhidi ya Watanzania ni changamoto,
ambayo hatuna budi kama taifa kuivalia njuga na kuona namna gani ya
uhakika na bora zaidi ya kuwakabili wenzetu hao, wanaotuchafulia sifa na
hadhi nzuri ya nchi yetu katika medani ya kimataifa.
Tungependa kutoa wito maalumu kwa maofisa wetu, wanaoshughulika na
udhibiti wa biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya, kuweka mikakati
mipya na yenye kuleta tija vilivyo katika vita dhidi ya biashara hii
haramu, ikiwa ni pamoja na kupatiwa nyenzo muhimu na za kisasa katika
vita hii ngumu lakini inawezekana kudhibitiwa.
Ni muhimu pia kuelewa kwamba madawa ya kulevya ni vita ngumu karibu
duniani kote kutokana na wahusika katika biashara hii kuwa na uwezo wa
kifedha, lakini hapa tungependa pia wananchi, viongozi mbalimbali na
jamii kwa ujumla kutoa kila aina ya ushirikiano kuwafichua watu
wanaojihusisha na biashara hii kwa sababu tunaishi nao katika maeneo
yetu mbalimbali.
Dawa za kulevya ni adui mkubwa duniani, hususan kwa vijana ambao
ndiyo walinzi wa taifa lolote lile makini na hivyo tuna kila sababu ya
kuwalinda vijana wetu dhidi ya kujihusisha na matumizi yake pamoja na
kufanya biashara ya kusafirisha kwenda nchi mbalimbali.
Sisi tunaamini kwamba umoja ni nguvu na tukitoa ushirikiano kwa
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, vinavyoshughulika na janga hili,
tutafanikiwa kudhibiti hali hiyo na kulinda hadhi na sifa ya taifa letu.
Tupambane nao mpaka kieleweke.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment