DENI la Taifa limezidi kupanda kutoka dola za Marekani bilioni 19. 69
Juni mwaka jana na kufikia Dola 23.2 ambazo ni zaidi ya Sh trilioni 51,
sawa na ongezeko la asilimia 18.
Katika deni hilo ambalo limeongezeka kwa asilimia 18, Serikali
inadaiwa Dola za Marekani bilioni 20.5 huku sekta binafsi zikiwa Dola
bilioni 2.7.
Taarifa ya kupanda kwa deni la taifa ilitolewa jana bungeni na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali
na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema).
Kubenea aliitaka Serikali ieleze ina deni kiasi gani na mikakati yake katika kukabiliana na ongezeko la deni hilo.
Katika swali lake, Kubenea alisema kuwa Serikali ya awamu ya nne
ilikopa fedha kwenye benki za nje za kibiashara, kwamba mwaka 2011
ilikopa Sh trilioni 15 na kufanya deni la taifa kufikia Sh trilioni 21
kabla ya mwaka 2015 na ilikopa tena Sh trilioni 9 na kulifanya kufikia
Sh trilioni 39.
Akijibu swali hilo la msingi, Dk. Kijaji alisema deni la Serikali
lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo, ikiwamo ya kimkakati ya kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya
umeme wa msongo wa KV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga, mabasi yaendayo
haraka, ujenzi wa bomba la gesi, mitambo ya kusafirisha gesi, upanuzi wa
Uwanja wa Ndege Dar es Salaam na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.
Alisema mikakati ya Serikali kukabiliana na deni hilo, ni pamoja na
kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,
kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya
kibiashara kwa miradi yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa pato la
taifa.
“Kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa makandarasi na
watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali
kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu,” alisema Dk.
Kijaji.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali ilipokea
mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara Sh trilioni 1.3 na
mwaka 2014/2015 ilipokea mkopo wa Sh trilioni 2.3. Mikopo hiyo
haikufikia Sh trilioni 15 kwa mwaka 2011 na trilioni 9 kabla ya mwaka
2015.
Kutokana na hali hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye
pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema kwa mujibu wa
takwimu hadi kufikia Juni mwaka huu deni la taifa ni zaidi ya Sh
trilioni 51, ambazo ukigawa kwa Watanzania kila mmoja anadaiwa zaidi ya
Sh milioni 1.
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kurejea katika Mpango wa Kusamehewa Madeni (HIPC).
Akijibu swali hilo, Dk. Kijaji alisema zipo nchi ikiwamo Iran na Iraq
zilikuwa katika mpango wa kusamehe madeni hayo, lakini kutokana na
migogoro katika nchi hizo hatua hiyo imeshindwa kufikiwa.
Swali hilo pia lilijibiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu
Nchemba ambaye alisema Serikali haikopi fedha kwa ajili ya matumizi ya
kawaida bali ni kwa shughuli za maendeleo ya nchi.
WADAU WAZUNGUMZIA
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo
Tanzania (TGDD), Hebron Mwakagenda, alisema kitendo cha kukopa mara kwa
mara lazima deni hilo liongezeke.
Alisema awali deni hilo lilifikia asilimia 38 na kwamba iwapo
litafikia asilimia 50, Serikali inapaswa kusimama kukopa hadi
watakapoanza kulipa madeni.
“Ikiwa deni la taifa limefikia asilimia 50, lazima tusimame kwanza
kukopa hadi tutakapoanza kulipa madeni hayo, la sivyo hakutakuwa na sifa
ya kukopa tena,” alisema Mwakagenda.
PROFESA NGOWI
Kwa upandewake mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na mchambuzi wa
masuala ya uchumi, Profesa Honest Ngowi, alisema kukua kwa kasi deni
hilo ni suala linalotisha.
“Jambo la msingi la kujiuliza ni kwanini deni linakua, linakua kwa
sababu tunakopa na tunakopa kwa sababu fedha za makusanyo yetu ya ndani
hazitoshi kwenda kutoa huduma mbalimbali kwa umma.
“Lakini kwa muda mrefu tumekuwa tunasema kwamba kati ya vitu
vinavyotisha si deni, bali ni kule kukua kwa kasi kwa deni hilo,”
alisema.
Profesa Ngowi alisema kukua kwa deni hilo kunatisha kwani jinsi
ilivyo linapaswa kulipwa, wakati fedha hizo zingeenda kuwekezwa kwenye
miradi mingine ya maendeleo.
“Kama nilivyosema deni linapaswa kulipwa, lakini inatisha kuona
linakua kwa kasi wakati huo huo lazima lilipwe, lakini kama fedha hizo
zilikopwa na kupelekwa kwenye maendeleo ni sawa… si mbaya. Lakini kama
hazikupelekwa kwenye shughuli za maendeleo itakuwa ‘isssue’,” alisema.
PROFESA SEMBOJA
Mtaalamu wa Masuala ya Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Profesa Haji Semboja, alisema kuendelea kukua kwa deni hilo ni
changamoto kwa Serikali iliyopo madarakani.
“Kwa kawaida nchi masikini hulazimika kukopa fedha kutoka nchi
nyingine kwa ajili ya kuziweka kwenye miradi ya maendeleo. Lakini kadiri
unavyochukua ikiwa uwezo wako wa kulipa deni ni mdogo, maana yake ni
kwamba mzigo wa deni unazidi kuongezeka,” alisema Profesa Semboja.
Alisema iwapo deni linaongezeka wakati fedha zikiwa zimewekezwa kwenye miradi ya maendeleo ni rahisi kulilipa.
“Lakini kama tulikopa kwa ajili ya shughuli zisizo za maendeleo, kwa ajili ya kula tu, ni hatari,” alisema.
Aliongeza: “Hata hivyo Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John
Magufuli imeanza vizuri, inasisitiza kuwekeza kwenye maendeleo, hiyo ni
sahihi kwa sababu nchi itapata fedha na mkiwa na miradi mingi ya
maendeleo ni rahisi kukopesheka zaidi.”
Hata hivyo, alisema Rais Magufuli ameonyesha nia ya kuwekeza kwenye
shughuli za kimaendeleo ikiwamo kilimo, ujenzi wa madaraja, barabara na
nyinginezo, ni vema akasimamia kwa dhati suala hilo ili kwamba fedha
zinazokopwa zitumike vile inavyopaswa kuwa.
“Tukichukulia mfano daraja la Kigamboni ni mradi mzuri wa maendeleo,
ingawa inaweza kuchukua muda mrefu kupatikana fedha za kulipa deni.
Lakini ndivyo inavyotakiwa, kwamba fedha ziwekezwe kwenye miradi na si
vinginevyo,” alisema.
ZITTO
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam, Kiongozi wa
Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema katika kipindi cha miezi
sita tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, uchumi wa taifa
umeporomoka kwa asilimia nne.
Akinukuu taarifa ya Benki Kuu (BoT), alisema katika kipindi cha
Oktoba hadi Desemba mwaka jana, pato la taifa lilikua kwa asilimia tisa.
Lakini kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, limepungua na kufikia
asilimia 5.5.
Alisema kulingana na mwenendo wa uchumi, Kamati Kuu ya chama hicho
imeitaka Serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha nchi.
Zitto alisema uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuitelekeza
Serikali kwa mwanasiasa mmoja na kudhani ndiye anayejua kila kitu na
kuwa mshauri wa washauri wa uchumi, itasambaratisha uwekezaji nchini na
kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia uwekezaji na kujenga uchumi
shirikishi.
“Tunawahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni
uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo msingi wa kuvutia uwekezaji
ni utawala bora. Serikali ya CCM inapaswa kujua kuwa kuua utawala wa
sheria ni kuua uwekezaji pamoja na uchumi wa nchini.
“Hali hiyo inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika
kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa awamu ya tano umepungua kwa
asilimia 4,” alisema Zitto.
Zitto ambaye alikuwa akitoa msimamo wa Kamati Kuu ya chama chake
iliyoketi mapema wiki hii Dar es Salaam, alisema katika sekta ya kilimo
ambayo hutegemewa na wananchi kwa asilimia 70, pato la uchumi limezidi
kushuka kutoka kasi ya ukuaji wa asilimia 10 kwa robo ya mwisho wa mwaka
jana hadi kufikia asilimia 2.7 katika kipindi cha Januari hadi Machi,
mwaka huu.
Aprili 21, mwaka huu wakati wa mkutano wa Bunge la bajeti,
Mwenyeikiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, alisema deni la taifa
limeendelea kukua na kufikia Sh trilioni 36.39 hadi kufikia Desemba
2015, ikiwa ni tofauti na ililivyokuwa Sh trilioni 14.4 kwa mwaka
2011/12.
“Kwa sasa deni limefikia takribani asilimia 44.9 ya pato la taifa,
limeendelea kukua kutokana na Serikali kuendelea kukopa kwa ajili ya
kugharimia nakisi ya bajeti,” alisema.
source:Mtanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment