UPELELEZI wa kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa jiji la Dar es
Salaam, Theresia Mbando inayowakabili wabunge watatu wa Chadema, akiwemo
wa Ubungo, Saed Kubenea, umekamilika.
Wakili wa Serikali, Flora Massawe amesema jana mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu, Huruma Shahidi, wakati kesi hiyo ilipotajwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kutokana na kukamilika kwa upelelezi, Wakili Flora aliiomba mahakama
iahirishe kesi hiyo hadi tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea
washitakiwa maelezo ya awali.
Mbali na Kubenea, wabunge wengine ni Halima Mdee (Kawe) Mwita Waitara
(Ukonga) na Diwani wa Kata ya Tabata Kimanga, Manase Mjema, aliyekuwa
Diwani wa Kata ya Kimara, Ephrein Kinyafu na mfanyabiashara Rafii Juma.
Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa hao kusomewa maelezo hayo ya awali.
Washitakiwa hao wanadaiwa Februari 27, mwaka huu, katika ukumbi wa
Karimjee, wilayani Ilala, kwa pamoja walimjeruhi Theresia na
kumsababishia majeraha katika vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi wa
meya na naibu wake wa Jiji la Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, kesi ya uhujumu uchumi na kuisababisha
serikali hasara ya Sh bilioni 1.16 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na
wenzake saba imeahirishwa hadi Oktoba 12, mwaka huu.
Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliahirisha kesi hiyo baada ya
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leornad
Swai kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Mbali ya Maimu, washitakiwa wengine ambao wote wapo nje kwa dhamana
ni Meneja Biashara wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Avelin Momburi,
Mkurugenzi wa TEHEMA, Joseph Makani.
Wengine ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula,
Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa
Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na
Xavery Kayombo.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kutumia madaraka vibaya,
kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na
kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment