Image
Image

Wazembe waadhibiwe kudhibiti vifo vya uzazi.


KATIKA toleo la jana, tulichapisha habari ikieleza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda, ameagiza kusimamishwa kazi na kufanyika kwa vikao vya kisheria ili kuwafukuza kazi watumishi wawili wa idara ya afya wilayani humo kwa uzembe ambao ungesababisha kifo cha mjamzito.

Mtanda alitoa agizo hilo baada ya mjamzito Catherine Gideon (33), mkazi wa kijiji cha Kasu wilayani humo, kujifungua kwa kupewa msaada na baadhi ya wagonjwa waliokuwapo hapo, ikiwa ni pamoja na kusaidiwa kukata kitovu cha mtoto na mjamzito mwenzake aliyekuwapo hospitalini hapo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mzazi huyo alifikwa na mkasa huo katika hospitali teule ya wilaya na baada ya kukosa huduma kutoka kwa muuguzi wa zamu, na muuguzi msaidizi, ambao inadaiwa kuwa hawakuwapo kazini tangu saa 4:00 usiku.
Mtanda anasema amechukua hatua za kinidhamu kutokana na watumishi hao kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Kwa mujibu wa DC Mtanda, watumishi hao walirejea kazini saa 12 alfajiri na kukuta wagonjwa wameshamsaidia mzazi.
Kutokana na manung’uniko kutoka kwa wagonjwa, ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuwaandikia barua za kuwasimamisha kazi sambamba na kuagiza vikao vya kisheria na nidhamu vianze kuketi kukutana ili kubaini makosa yao na kuwachukulia hatua.
Matukio ya wajawazito kukosa huduma za msingi kutoka kwa watoa huduma wakiwamo wauguzi na wauguzi wasaidizi yamekuwa yakitajwa sana kwamba yanachangia kasi ya vifo vya wajawazito nchini.
Ripoti ya Benki ya Dunia mwaka huu inaonyesha kwamba wajawazito 1,255 nchini hufariki dunia kila mwezi, wastani wa wajawazito 42 hupoteza maisha kila siku wakati wajawazito wawili kufariki kila saa.
Takwimu hizi zinatisha na zinatoa somo kwamba Tanzania kama taifa haijaweza kuchukua hatua zinazostahili katika kudhibiti vifo vya wajawazito na watoto.
Itakumbukwa kwamba suala la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto ni moja ya ajenda za Malengo ya Millenia, hivyo msukumo unahitajika ili kufikia lengo hilo katika muda mwafaka 2025.
Tutaweza kudhibiti vifo vya wajawazito na watoto au kuvipunguza kwa kiwango kikubwa kwa kuhakikisha kwamba huduma zinaboreshwa zikiwamo za dawa na vifaa tiba katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zote.
Suala la nidhamu na maadili kwa watumishi ni miongoni mwa mambo muhimu katika kutoa huduma bora kwa wajawazito na watoto. Vifaa tiba na dawa vinaweza kuwapo, lakini kama watoa huduma hawatakuwa na nidhamu, maadili ya utumishi wa umma na ya kitaaluma huduma bora haziwezi kupatikana na ni dhahiri kuwa zitakuwa ndoto kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
Tukio la Rukwa ni mfano dhahiri wa baadhi ya watoa afya kutokuwajibika katika kutekeleza majukumu yao na linatoa picha kuwa vitendo kama hivyo vinachangia vifo vya wajawazito na watoto visiyo vya lazima.
Mamlaka husika zinapaswa kufuatilia na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za watoa huduma za afya ambao watabainika kutowajibika na kukiuka maadili ya kazi na ya kitaaluma kama alivyofanya Mtanda.
Pia, kuna haja ya kupeleka mahitaji muhimu kama dawa, vifaa tiba na watoa huduma za afya wa kutosha katika maeneo ya vijijini ambayo yakakabiliwa na changamoto hizo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment