SIMBA jana iliendelea kuwapa raha mashabiki wake baada ya kuifunga
Toto Africans mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye
Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo izidi kujichimbia kileleni mwa
msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 katika mechi 11 ilizocheza huku Toto
ikibaki mkiani ikiwa na pointi zake nane katika mechi 12.
Mara kadhaa Toto huisumbua Simba zinapokutana, msimu uliopita
zilitoka sare katika mechi ya kwanza na timu hiyo ya Mwanza kuibuka na
ushindi katika mechi ya marudiano.
Muzammil Yassin ndiye aliyeanza kuamsha shangwe za mashabiki wa Simba
baada ya kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 43 kwa kuunganisha
pasi nzuri ya Fredrick Blagnon.
Toto walicheza mchezo wa kuzuia karibu muda wote wa kipindi cha
kwanza, hali iliyosababisha kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao hilo
moja.
Dakika chache baada ya kuanza kipindi cha pili Blagnon alilazimika
kutoka baada ya kuumizwa na beki wa Toto na hivyo nafasi yake
kuchukuliwa na Laudit Mavugo.
Mavugo raia wa Burundi hakufanya kosa kwani katika dakika ya 52
aliiandikia Simba bao la pili. Alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi
safi ya Mohamed Ibrahim ‘Mo’na kuunganisha mpira moja kwa moja nyavuni
na kumuacha kipa wa Toto Mussa Kirungi asijue la kufanya.
Muzammil aliwanua tena mashabiki wa Simba katika dakika ya 74
alipofunga bao la tatu kwa kuunganisha mpira wa kona uliochongwa na Said
Ndemla na mpira kwenda moja kwa moja wavuni.
Katika mechi nyingine ya ligi iliyochezwa jana kwenye uwanja wa
Sokoine Mbeya wenyeji Prisons walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbao.
Matokeo hayo yanaifanya Prisons kufikisha pointi 16 na Mbao pointi 13
katika msimamo wa ligi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment