MWANAFUNZI
wa kidato cha tatu, katika Shule ya Sekondari ya Kutwa Mbeya (Mbeya Day) ya
jijini hapa, Sebastian Chinguku (17), amefanyiwa ukatili kwa kuchapwa fimbo na
makofi na walimu wanne.
Tukio
hilo la kusikitisha, lilitokea shuleni hapo Septemba 28 mwaka huu, katika ofisi
ya walimu shuleni hapo na lilifahamika kuanzia jana kupitia mitandao mbalimbali
ya kijamii.
Walimu
waliohusika kumchapa mwanafunzi huyo, wamefahamika kuwa ni Franky Msigwa, Deo
John na Evance Sanga kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE) na
Sanke Gwamaka kutoka Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Taarifa
zilizopatikana zinasema kwamba, wakati walimu wakimpiga mwanafunzi huyo,
mwalimu mwenzao aliyetambulika kwa jina la Esther Harembo kutoka Chuo Kikuu cha
Iringa, alikuwa akiwazuia wenzake hao wasimpige mwanafunzi huyo, huku akiwapiga
picha na kuwarekodi kwa simu ya mkononi.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, walimu hao walikuwa mafunzoni kwa vitendo shuleni hapo
kwa kipindi kadhaa.
Pia
inasemekana, walimu hao walimpiga Sebastian baada ya kushindwa kufanya kazi ya
somo la kiingereza iliyokuwa imetolewa na Mwalimu Msigwa Septemba 26, mwaka
huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Katibu Tawala, Mkoa wa Mbeya (RAS), Mariam
Mtunguja, alisema kabla mwanafunzi huyo hajapigwa na walimu wake, Mwalimu
Msigwa alimpiga kofi baada ya kushindwa kuelewana.
“Siku ya
tukio, inasemekana Mwalimu Msigwa alifika darasani na kutaka kujua wanafunzi
ambao hawakufanya kazi aliyokuwa ametoa.
“Wanafunzi
walijitokeza akiwamo Sebastian ambaye alijitetea kwamba hakuwapo shuleni wakati
kazi hiyo inatolewa, hivyo akaomba asamehewe.
“Inavyoonekana,
Mwalimu Msigwa hakumwelewa mwanafunzi wake, hivyo akampa adhabu ambayo
aliikataa kisha akamwambia apige ‘pushapu’ na baadaye akampiga kofi.
“Mwanafunzi
alipopigwa alihoji ni kwanini amepigwa wakati hakuwa na kosa, jambo ambalo
lilimuudhi mwalimu huyo na kuamua kuwaita walimu wenzake ili wamsaidie
kumwadhibu.
“Wale
walimu walioitwa, walikuja na wakamchukua Sebastian hadi ofisini ambako
walianza kumpiga fimbo bila utaratibu kama inavyoonekana katika picha za
mitandao ya kijamii.
“Lakini,
kwa sasa walimu hao wameshaondoka shuleni hapo na kurudi katika vituo vyao vya
masomo baada ya muda wao kumalizika mwishoni mwa mwezi uliopita,” alisema
Mtunguja huku akishangaa ni kwanini mkuu wa shule hiyo hakutoa taarifa katika
vyombo vinavyohusika.
Wakati
Mtunguja akieleza hayo, kiongozi wa darasa analosoma Sebastian, Venance
Kibanda, alisema yeye na wanafunzi wenzake walisikitishwa na adhabu aliyopewa
mwenzao kwa sababu ilikuwa kubwa ikilinganishwa na kosa alilodaiwa kufanya.
“Mwenzetu
alimwomba mwalimu ampe nafasi ya kufuata kibali alichopewa na mwalimu wa darasa
kuonyesha kwamba siku iliyotolewa kazi, hakuwapo shuleni.
“Wakati
anataka kutoka nje, Mwalimu Msigwa alimzuia mlangoni na kuwaita walimu wenzake
watatu ambao walifika na kuanza kumwadhibu huku wakimpeleka katika ofisi ya
walimu ambako walimpiga kwa fimbo, ngumi na mateke bila huruma.
“Baada ya
kumpiga hivyo, walimrudisha darasani kutuonyesha jinsi walivyomwadhibu mwenzetu,”
alisema Kibanda.
Mkuu wa
Shule hiyo, Magreth Haule, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alisema siku ya
tukio hakuwapo shuleni na kwamba majukumu yote alimkabidhi makamu wake, Adonath
Nombo.
Naye
Nombo alipozungumzia suala hilo, alisema wakati walimu wanampiga mwanafunzi
huyo, alikuwa kwenye kikao cha wazazi pamoja na baadhi ya walimu.
“Wakati
wa tukio nilikuwa kwenye kikao ila majukumu yote niliyaacha kwa walimu hao wa
mazoezi,” alisema Mwalimu Nombo.
Baba
mzazi wa mwanafunzi huyo, John Chinguku, alipohojiwa juu ya tukio hilo,
alionyesha kukerwa na kusema anamwachia Mungu pamoja na Serikali.
“Mwanangu
ambaye ni pacha, namfahamu tabia yake, lakini adhabu aliyopewa ni kubwa,”
alisema Chinguku kwa kifupi.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema
wanawashikilia walimu saba wa shule hiyo akiwamo mkuu wa shule.
“Mkuu wa
shule, baadhi ya walimu na wanafunzi, tunawashikilia kwa ajili ya mahojiano.
Wale waliohusika kumpiga mwanafunzi, bado hatujawakamata, lakini tunawatafuta,”
alisema Kamanda Kidavashari.
WAZIRI WA
ELIMU.
Naye
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ametangaza
kuwafukuza chuo walimu hao waliompiga mwanafunzi huyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri Profesa Ndalichako
alisema kitendo kilichofanywa na walimu hao ni cha kikatili kisichoweza
kuvumilika.
“Tumechukua
uamuzi wa kuwafukuza mara moja kwa kuwa walimu hawa wanafunzi hawafai kuendelea
na taaluma hii wakati hatua zaidi za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi
yao.
“Lakini,
natoa onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mazoezi ya vitendo, wasiende
kinyume na taaluma kwani wakifanya hivyo watakuwa wanapoteza sifa za kuwa
walimu,” alisema Profesa Ndalichako.
WAZIRI WA
MAMBO YA NDANI
Wakati
hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema
ameviagiza vyombo vya dola jijini Dar es
Salaam, viwatafute walimu hao na kuwakamata.
“Nimeelekeza
vyombo vya dola viwatafute chuoni na popote walipo. Taarifa zaidi za tukio hilo
zinasema wakati mwanafunzi huyo anapigwa, Mwalimu Esther Harembo wa Chuo Kikuu
cha Iringa, ndiye aliyekuwa akizuia mwanafunzi asipigwe na ndiye aliyekuwa
akisema mwacheni mtamuumiza huku akichukua video,” alisema Nchemba.
WAZIRI
SIMBACHAWENE.
Nayo Mamlaka
ya Nidhamu kwa Walimu, imeagizwa kumvua madaraka Mkuu wa Shule hiyo, kwa sababu
ya kushindwa kutoa taarifa ya tukio
hilo.
Kauli
hiyo, imetolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George
Simbachawene.
“Ninaagiza
mamlaka husika za kinidhamu kumvua madaraka Mwalimu Magreth kutokana na kukaa
kimya huku kukiwa na tukio la unyama dhidi ya mwanafunzi,”alisema Simbachawene.
Pamoja na
hayo, alisema Serikali imeshachukua hatua kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa
wa Mbeya, kuendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo.

0 comments:
Post a Comment