KLABU ya Yanga imetangaza kuwapo kwa Mkutano Mkuu wa dharura Oktoba 23 mwaka huu.
Mkutano huo unakuja huku ikiwa ni siku chache baada ya serikali
kukataa kuikodisha timu hiyo kwa mfanyabiashara maarufu nchini Yusuf
Manji ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu hiyo.
Klabu hiyo juzi ilithibitisha kukodishwa kwa mfanyabiashara huyo,
ikiwa ni siku chake baada ya kuikabidhi klabu eneo la miradi wa ujenzi
wa uwanja huo lililopo Kigamboni.
Kwa sasa uongozi wa klabu hiyo utakutana na wanachama huku ajenda za
kikao hicho zikiwa hazifahamiki na wala haujulikani utafanyikia wapi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Yanga ilisema kuwa bado
wanachama wataarifiwa kuhusu ajenda za kikao chao hicho kadiri siku
zinavyozidi kwenda mbele.
Lakini pia taarifa hiyo ilisema kuwa wanachama watataarifiwa baadaye
kuhusu mahali ambapo mkutano huo utafanyika, kwa kuwa kwa sasa bado ni
mapema. Juzi kupitia Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa
(BMT) Mohamed Kiganja, Serikali ilitangaza kutotambua kukodishwa kwa
Yanga kwa Manji kupitia kampuni yake ya Yanga Yetu.
Kiganja alisema kuwa Yanga walikodi klabu hiyo bila kufuata taratibu
zinazokubalika na BMT pamoja na Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo
nchini na ndio maana zoezi hilo ni batili. Yanga imekodisha klabu yao
hiyo kwa Manji kwa kipindi cha miaka 10, ambapo itakuwa chini ya tajiri
huyo atakayeihudimia kwa kila kitu kwa mujibu wa makubaliano.
Mapema jana, Baraza la Wadhamini wa Yanga lilimjibu Kiganja likisema
kuwa kabla ya uamuzi wa kuikodisha timu kwa kampuni ya Yanga Yetu,
lilipata msaada wa kisheria kutoka kwa magwiji wa sheria nchini.
Ilielezwa kuwa baada ya kuandaa muswada wa kukodisha timu kwa pamoja
na wakodishwaji, waliupeleka kwa wanachama wao ambao magwiji wa sheria
nchini kuomba msaada wa kisheria, ambao walitoa ushauri.
Kiujumla, Baraza la Wadhamini wa Yanga linasisitiza kuwa utaratibu wa
kuikodisha Yanga kwa Manji ulifuata taratibu zote tofauti na Kiganja
anavyosema. Yanga kimsimamo kwa sasa ipo nafasi ya sita katika Ligi Kuu
Tanzania Bara ikiwa na pointi 11, Simba inaongoza Ligi hiyo ikiwa na
pointi 17 huku Stand United ikiwa na pointi 16.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment