Image
Image

Majaliwa awataka viongozi wa dini kuhimiza waumini wao kujiepusha na vitendo vya chuki.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa dini nchini, kutimiza wajibu wao kwa kuwahimiza waumini wao kujiepusha na kauli na vitendo vitakavyopandikiza chuki na uchochezi miongoni mwa waumini wa dini moja dhidi ya waumini wa dini nyingine.
Alitoa kauli hiyo jana mkoani hapa, wakati akihutubia kwenye Baraza la Maulid lililofanyika Shelui.
Pamoja na hayo, alisema Serikali ya awamu ya tano ipo imara na haitayumba.
“Ni vema tukatambua kwamba, katika mifarakano na uhasama wa kidini, hakuna atakayeibuka mshindi bali wote tutakuwa ni watu tulioshindwa.
“Nyumba za ibada zisaidie kuunganisha waumini na kuwa mfano usoni kwa jamii, kwa sababu mara kadhaa watu wameshuhudia migogoro na mapigano katika misikiti wakigombea uongozi na mali, matukio ambayo hayana tija ndani ya Uislamu.
“Kwa hiyo, ni vema mkafuata misingi ya dini ya kuheshimiana, kuelewana na kuvumiliana na tumieni mabaraza kukemea hali hiyo inayowagawa Waislamu,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema Serikali itaendelea kuzitegemea dini zote katika kujenga misingi imara ya kuleta amani miongoni mwa Watanzania.
“Pia, Serikali itaendelea kusisitiza na kuheshimu uhuru wa raia wa Tanzania kuabudu dini wanayoiamini, kwa sababu ni moja kati ya haki za msingi za kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kufanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba uhuru huo unaheshimiwa, kwa sababu hiyo ni nyenzo muhimu iliyosaidia kulifanya taifa letu kuwa mfano wa kuigwa kote duniani.
“Tutaendelea kushirikiana na viongozi wa dini zote nchini, ili kuhakikisha tunu hiyo muhimu haichezewi na mtu au kikundi chochote,” alisema.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuwapo kwa tishio la ugaidi duniani ambalo limegharimu maisha ya baadhi ya wananchi.
“Hapa mmezungumzia kuhusu uwezekano wa baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi kufunguliwa mashtaka kwa sababu ya chuki au kulipiza kisasi.
“Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali iko macho katika kupambana na tishio lolote la kiusalama ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
“Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya utayari wakati wote ili kupambana na vikundi au watu na mtu yeyote mwenye nia ya kuhatarisha usalama wa nchi yetu,” alisema.
Pamoja na hayo, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa dini, kwamba jukumu la ulinzi wa nchi kwa mujibu wa Katiba ni la kila mwananchi, na kwamba kila mmoja anatakiwa kulinda amani popote alipo.
“Katika hili, ni vema viongozi wa dini mkatambua kwamba nyinyi pamoja na waumini mnaowaongoza, ndio walinzi wa taifa na mnalo jukumu la kuendelea kuwasihi waumini kuendelea kuwa raia wema na kutoa taarifa za dalili za uhalifu mapema iwezekanavyo.
“Kwa mfano, hawa watoto wanaojiita Panya Road huko Dar es Salaam au vijana wanaoteka magari pale Mlima Sekenke. Hao hawatoki kwenye sayari nyingine bali ni watoto wetu na tunaishi nao majumbani, tunaabudu nao misikitini au makanisani.
“Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwaripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili watambulike na washughulikiwe ipasavyo ili wasiendelee kuleta madhara kwa raia wema,” alisema.
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu  Abubakari Zuberi bin Ally, aliwaomba Waislamu nchini waishi kama alivyokuwa akiishi Mtume Muhammad (S.A.W), ambaye alisisitiza kupendana na kushikamana na kuwajali wengine bila kuwabagua kiimani.
“Si jambo rahisi kupata kipato bila kufanya kazi, tutalaumu kila siku kuwa hatuoni mabadiliko ya kipato wakati sisi wenyewe hatufanyi kazi.
“Uislamu ni kielelezo tosha kwa mfano wa maisha bora, si kweli kuwa dini yetu inafundisha tuchukie wengine.
“Waumini wa dini zote shikeni imani iliyo sahihi na puuzeni kauli za baadhi ya watu wanaosema magaidi hutokea katika dini ya Kiislamu kutokana na kuwa na imani kubwa ya Kiislamu,” alisema Mufti Zuberi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema Serikali itaendelea kupambana na watu ambao wamekuwa wakienda kinyume na sheria za nchi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment