Image
Image

Ufaulu kidato cha nne juu, shule 6 za Dar es Salaam zaburuza mkia.

WAKATI Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) likitangaza matokeo ya Kidato cha Nne kwa mwaka 2016 na kuonesha ufaulu wa jumla kwa watahiniwa wa shule umeongezeka kwa asilimia 2.44, idadi ya watahiniwa waliopata alama za kuwawezesha kuendelea na kidato cha tano imekuwa chini kwa miaka mitatu mfululizo.
Matokeo ya mtihani uliofanyika Novemba, 2016 na kutangazwa 31 January 2017 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, yanaonesha watahiniwa wa shule 244,762 ambayo ni asilimia 70.35 ya waliofanya mtihani walifaulu mtihani huo.
Ufaulu huo unaonesha kuongezeka kwa asilimia 2.44 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2015 ambayo wanafunzi 240,996 ambao ni asilimia 67.91 walifaulu na kwa mwaka 2014 walikuwa ni 169,642 (asilimia 69.76) na mwaka 2013 walikuwa ni 201,152 ambao ni asilimia 57.09.
Jumla ya watahiniwa 408,372 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2016, wakiwemo wasichana 209, 456 sawa na asilimia 51.29 na wavulana 1998, 916 (asilimia 48.71).
Kati yao wote waliosajiliwa, watahiniwa wa shule walikuwa 355,822 na wa watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 52,550. Ufaulu kwenda Kidato cha V Pamoja na ufaulu huo kuongezeka, inaonesha kuwa watahiniwa wanaopata madaraja yanayoweza kuwafanya wakaingia kidato cha tano (daraja la I-III), inaonekana kuwa chini ya asilimia 50.
Kwa matokeo ya mwaka jana, watahiniwa 96.018 ambao ni asilimia 27.60 wamepata daraka la I-III, wakati mwaka 2015 walikuwa ni 89,929 ambayo ni asilimia 25.34 na mwaka 2014 walikuwa ni 73,832 ambao ni asilimia 30.72.
Watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 32,521 sawa na asilimia 68.19. mwaka 2015 walikuwa ni 31,1951 sawa na asilimia 64.80, hivyo ufaulu kuongezeka kwa asilimia 3.39. Kwa upande wa maarifa, watahiniwa 8,751 sawa na asilimia 50.48 wamefaulu, mwaka 2015 watahiniwa 7,536 ambao ni asilimia 46.63 hivyo kuwapo ongezeko ya ufaulu kwa asilimia 3.85.
Kuhusu ufaulu wa masomo unaonesha kuwa masomo ya Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Hisabati, Fizikia, Biolojia, Commerce na Book-Keeping umepanda kwa asilimia 0.12 na asilimia 8.08 ikilinganishwa na mwaka 2015.
Watahiniwa wanaonekana kufanya vizuri zaidi kwenye somo la Kiswahili ambapo ufaulu wake ni asilimia 77.75 ya watahiniwa wote, ingawa ufaulu huo umeonekana kushuka ukilinganisha na mwaka 2015 uliokuwa ni asilimia 77.63 na mwaka 2014 ulikuwa asilimia 69.66.
Aidha, watahiniwa wameshindwa kufanya vizuri katika somo la Hisabati ambalo pamoja na kuonekana ufaulu umeongezeka waliofaulu somo hilo ni asilimia 18.12 ya watahiniwa wote wa shule, mwaka 2015 walikuwa ni asilimia 16.76 na mwaka 2014 ilikuwa ni asilimia 19.58.
“Pamoja na asilimia ya ufaulu wa jumla kuendelea kuimarika, takwimu zinaonesha kuwa bado ufaulu wa masomo na watahiniwa waliopata daraja la I-III ni chini ya asilimia 50, hivyo juhudi za makusudi zinahitajia kuendelea kufanya ili kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo na kuongezeka kwa idadi ya watahiniwa kwenye madaraja ya ufaulu,” alisema Dk Msonde.
Shule za binafsi vinara
Kuhusu upangaji wa matokeo kwa shule zenye wanafunzi zaidi ya 40, unaonesha shule za watu binafsi na mashirika ya dini zimeendelea kufanya vizuri katika nafasi za 10 bora kitaifa huku zile zinazomilikiwa serikali zikiendelea kufanya vibaya kwa miaka mitatu mfululizo.
Shule 10 Bora ni Feza Boys (Dar es Salaam), St Francis Girls (Mbeya), Kaizirege Junior (Kagera), Marian Girls, Marian Boys na St Aloysius Girls (Pwani), Shamsiye Boys (Dar es Salaam), Anwarite Girls (Kilimanjaro), Kifungilo Girls (Tanga) na Thomas More Machrina (Dar es Salaam).
Aidha, Mkoa wa Dar es Salaam umezorota kielimu baada ya kuwa na shule sita kati ya 10 zilizoshika nafasi za mwisho. Shule hizo ni Kitonga na Nyeburu (Dar es Salaam), Masaki (Pwani), Mbopo, Mbondole na Somangila Day (Dar es Salaam), Dahani (Kilimanjaro), Ruponda (Lindi), Makiba (Arusha) na Kidete (Dar es Salaam).
Mikoa iliyofanya vizuri katika nafasi ya 10 bora ni Njombe, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Tabora wakati halmashauri 10 bora ni Bukoba Mjini, Njombe Mjini, Kakonko, Kahama Mji, Wanging’ombe, Ilemela, Iringa Mjini, Mkuranga, Igunga na Kibaha Mji.
Ufaulu kwa watahiniwa 10 bora waliofanya vizuri kitaifa unaonesha kuwa ni asilimia 50-50 kwa wavulana na wasichana huku mwaka 2016 wakiongozwa na mvulana. Mwaka 2015, watahiniwa wa kike walikuwa ni wanne na wavulana sita na mwaka 2014 walikuwa na uwiano sawa, lakini waliongozwa na mwanafunzi wa kike.
Mvulana aongoza, msichana achomoza
Kwa 2016, watahiniwa 10 bora ni Alfred Shauri (Feza Boys), Cynthia Mchechu (St Francis Girls), Erick Mamuya (Marian Boys), Jigna Chavda (St Mary Goreti), Naomi Tundui (Mariam Girls), Victoria Chang’a (St Francis Girls), Brian Johnson (Marian Boys), Esther Mndeme (St Mary’s Mazinde Juu), Ally Koti (ALCP Kilasara) na Emmanuel Kajege (Marian Boys).
Watahiniwa wasichana 10 bora ni Cynthia, Jigna, Naomi, Victoria, Esther, Christa Edward (St Francis Girls), Nelda John (Marian Girls), Mariana Shabani (Kifungilo Girls), Beatrice Mwella (St Mary’s Mazinde Juu) na Rachel Kisasa (Canossa).
Wavulana 10 bora kitaifa ni Alfred, Erick, Brian, Ally, Emmanuel, John Ng’hwaya (Nyegezi Seminary), Clever Yohana (Livingstone Boys Seminary), Desderius Rugabandana (Morning Star), Kennedy Boniface na Assad Msangi (Feza Boys).
126 wafutiwa, 40 matokeo yazuiwa
Katika hatua nyingine, Dk Msonde alisema Necta limezuia matokeo ya watahiniwa 33 waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani katika baadhi ya masomo, pia matokeo ya watahiniwa 124 waliopata matatizo ya kiafya na kufanya masomo yote, watahiniwa wamepewa fursa ya kufanya mitihani wa Kidato cha Nne 2017.
Alisema pia baraza limezuia matokeo ya wanafunzi 40 wa Shule ya Sekondari ya Hellens wanaodaiwa alama endelevu hadi hapo mkuu wa shule atakapowasilisha alama hizo huku likifuta matokeo ya watahiniwa 126 waliobainika kufanya udanganyifu akiwamo mmoja aliyeandika matusi katika karatasi ya majibu.
Kati ya waliofutiwa matokeo 58 ni wa kujitegemea na 58 ni wa shule, 10 watihani wa maarifa. Mvulana kinara anena Akizungumza na gazeti hili, mwanafunzi bora kitaifa, Alfred Shauri alisema siri ya mafanikio yake ni bidii na kumtanguliza Mungu.
Alfred ambaye pia amefanya vizuri kwenye insha ya Afrika Mashariki alisema: “Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufikia ndoto yangu ya kufanya vizuri na nitaendelea kufanya bidii kwenye masomo, ingawa kufanya vizuri kidato cha nne haikupi njia ya kufanya vizuri kwenye mitihani ya elimu ya juu kama hujitumi.”
Kijana huyo ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne, anasema pamoja na wazazi wake kumtaka kufanya masomo ya sayansi ili kuwa mhandisi, ingawa anapenda fani hiyo, lakini angependa kujikita zaidi katika kuwekeza kwenye biashara na ujasiriamali. Mama yake Alfred, Adela Shauri pamoja na kumpongeza mwanawe, alisema mtoto wake ni kijana mwenye upendo na huruma ambaye anapenda kujibidisha kwenye masomo au kwa kile anachikifanya.
“Yaani mpaka nimetetemeka niliposikia haya matokeo, lakini niseme ni mtoto mwenye bidii katika masomo na anayemtangulia Mungu katika kila jambo. Niwaombe wazazi wenzangu kuhakikisha tunawalea watoto wetu wakiwa na hofu ya Mungu, kwani peke yetu hatutaweza,” alisema.
Kwa upande wa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili kitaifa na akiwa ni mwanafunzi bora kwa upande wa wasichana, Cynthia Mchechu alisema: “Mpaka sasa siamini haya matokeo, natamani kama nikalale hivi. Lakini nashukuru sana Mungu, kwani bidii katika masomo ndiyo imemfanya kufikia hapo.”
Msichana bora haamini
Cynthia anawashauri wanafunzi wenzake kuhakikisha wanatimiza ndoto zao kwa kujibidiisha na kuhakikisha wanakamilisha kile wanachotaka kupata katika maisha.
Naye Mercy Mchechu, mama mzazi wa Cynthia ambaye ni mtoto pekee wa kike kwake na mumewe Nehemia Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), anasema mwanawe amekuwa na juhudi ya masomo tangu akiwa anasoma shule ya awali na msingi Rightway ya Dar es Salaam ambayo yeye ndiye mkurugenzi wake.
“Ni binti ambaye ana bidii katika masomo na ana uwezo wa kutambua kile anachokitaka maishani na akaweza kutekeleza,” alisema Mercy.Matokeo yako hapa->http://necta.go.tz

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment