Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Ligi ya Mpira wa Kikapu (RBA) inayojumuisha timu 16 za wanaume na timu 8 za wanawake imepangwa kuanza Februari 11 na kumalizika Agosti 1 mwaka huu.
Ratiba hiyo imetangazwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu (Dar es Salaam),Bw. Okale Emesu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ufunguzi wa ligi hiyo.
Emesu amesema kuwa mashindano hayo yatafunguliwa katika uwanja wa Taifa na yataendelea kufanyika katika viwanja vingine vya Gymkhana na Donbosco-Upanga hivyo watakuwa wakitangaza mahali pa kuchezea mechi kabla ya siku husika.
“Mfumo wa ligi utakuwa wa nyumbani na ugenini katika hatua ya awali ambapo timu nane (8) za wanaume za nafasi za juu zitacheza mtoano (playoffs) hadi kupata bingwa. na kwa upande wa wanawake timu itakayokuwa nafasi ya kwanza ndio itakayotwaa ubingwa,”alisema Emesu.
Amezitaja timu za kiume zitakazoshiriki kuwa ni JKT, Savio, ABC, Vijana, Oilers, Pazi, Magereza, Donbosco youngsters, Mgulani, Magnet, Jogoo, Chui, Mabibo bullets, UDSM Outsiders, Ukonga Kings pamoja na Kurasini heat.
Kwa upande wa timu za wanawake, timu zitakazoshiriki ni JKT, Jeshi Stars, Vijana Queens, Donbosco lioness, Ukonga queens, Kurasini dIvas, Oilers princess pamoja na Prisons.
Akifafanua Emesa amesema kuwa, bingwa wa mashindano hayo atapata kikombe na fedha taslimu shilingi 5,000,000 vile vile mshindi wa pili na watatu pamoja na wachezaji bora watapewa zawadi.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa chama hicho, Peter Mpangala amesema kuwa kuna wadhamini wamevutiwa na mwongozo wao wa ligi hiyo na kuamua kuwadhamini hivyo bado wako katika mazungumzo.
“Mpaka sasa mdhamini ambaye tunae ni Azam pekee hivyo tunaomba wadhamini wengine waendelee kujitokeza ili tuweze kuendeleza ligi yetu ya mkoa na kukuza mchezo huu kwa ujumla,”alisema Mpangala.
Katika mikakati yao ya kupeleka mchezo kibiashara, chama hicho kimeanzisha mfumo mpya wa mikataba baina ya wachezaji na timu ambapo mkataba huo unaelezea kuhusu uhamisho wa mchezaji toka timu moja kwenda nyingine.
Aidha, uhamisho huo utahitaji malipo ambayo yatafanyika kulingana na thamani ya mchezaji ambapo mchezaji atapata asilimia 40 ya malipo hayo,timu pia itapata asilimia 40 na asilimia 20 zitaenda kwenye chama hicho.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment