Mkemia mkuu kuendelea na mafunzo kwa wadau Kanda ya Mashariki .
Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) wamejipanga kuendelea kuendesha mafunzo kwa wadau wa Kanda ya Mashariki wanaohusika na kemikali ili kuhakikisha kemikali zinatumika vema na kwa njia salama.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wasafirishaji na watumiaji wa kemikali nchini.
Prof. Manyele amesema kuwa wakala hufanya usajili na ukaguzi kwa wadau wote wanaohusika na kemikali wakiwemo waagizaji, watengenezaji, wasafirishaji, watumiaji, wanaosafirisha nje ya nchi au yeyote yule anayehusika na kemikali kwa njia moja au nyingine.
Pia ukaguzi huo unahusisha mahali ambapo kemikali zinatumika, zinatunzwa au kuhifadhiwa.
“Kuanzia mwaka 2012 hadi sasa, wadau wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani waliopatiwa mafunzo ni 642 wakiwemo Askari wa Jeshi la Polisi Usalama Barabarani Tanzania Bara, wasimamizi wa shughuli za uzalishaji kwenye viwanda, wasambazaji, wasafirishaji wa kemikali pamoja na madereva wanaosafirisha kemikali., hivyo baada ya kuona umuhimu wake tumeamua kuendelea na mafunzo haya kwa wadau wetu wengine,” alisema Prof.Manyele.
Prof. Manyele ameongeza kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa siku mbili kwa kila kundi katika makundi matatu yakiwemo ya wasimamizi wa shughuli zinazohusisha kemikali watakaoanza tarehe 21- 22/02/2017, Mawakala wa Forodha watakaoanza tarehe 23-24/02/2017 pamoja na madereva wanaosafirisha kemikali kuanzia tarehe 10-11/03/2017.
Aidha, Wakala Mkuu wa Serikali amefafanua kuwa Wakala hautaruhusu mdau ambaye hajapitia mafunzo hayo kuhusika katika shughuli yoyote ya kemikali kwa kutumia, kuhifadhi, kusafirisha, kutoa bandarini na hata kuagiza kutoka nje ya nchi hivyo akasisistiza umuhimu wa wahusika kuhudhuria mafunzo hayo.
Ametoa rai kwa wadau hao kuwahi kuhudhuria mafunzo haya ili kutekeleza matakwa ya Sheria Na. 3 ya mwaka 2003 ya Udhibiti na Usimamizi wa kemikali pamoja na kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza kwa sababu ya kukosa mafunzo.
0 comments:
Post a Comment