Gazeti hili toleo la jana kulikuwa na habari iliyomnukuu Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba akitishia kuwa chama hicho kitatangaza mgogoro na Serikali iwapo haitawalipa madai yao ya zaidi ya Sh800 bilioni.
Mukoba katika taarifa yake alitoa muda hadi mwisho wa mwezi huu Serikali iwe imewalipa madai yao na kama hawatakuwa wamelipwa Machi Mosi watatangaza mgogoro wa kazi na Serikali bila ya notisi nyingine kutolewa. Alisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha baraza la chama hicho kilichofanyika mkoani Morogoro hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Mukoba kati ya fedha wanazodai, zaidi ya Sh300 bilioni ni kwa ajili ya kuwalipa walimu stahili inayohusiana na kupandishwa madaraja, pia walimu 80,000 waliopandishwa madaraja kati ya Januari na Aprili 2016 hawajarekebishiwa mishahara yao.
Pia, alifafanua madai mengine ni Sh480 bilioni za walimu wastaafu wanaofikia 6,044 ambao wamekuwa wakidai tangu mwaka 2012 na kuna walimu 39,000 wanaopaswa kupandishwa madaraja katika mwaka huu wa fedha kuanzia Julai 2016, lakini hawajapandishwa hadi sasa.
Tunakubaliana na hoja ya Baraza la CWT kwamba walifikia uamuzi huo baada ya kuona madai ya walimu yanazidi kukua kwa kasi, kiasi kwamba hatua za haraka zisipochukuliwa hayatalipika.
Pia, tunashindwa kukubaliana na hoja iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ya kuwaomba walimu warudi mezani kwa ajili ya mazungumzo.
Hatuoni haja ya mazungumzo kwa sababu madai ya walimu yamekuwa ni wimbo wa miaka nenda rudi, lazima ifike mahala Serikali imalizane nao.
Tunachoona hapa kutolipa stahili za walimu kuna hasara nyingi zinazosambaa kitaifa, kubwa zaidi walimu hawa wamekuwa wakitumia muda mwingi kufikiria madai yao badala ya kufundisha na madhara yake kiwango cha elimu kwa wahitimu wengi ni duni.
Ni imani yetu kwamba hata matokeo duni ya ufaulu wa kidato cha nne ya hivi karibuni kwa shule za Serikali inawezekana ilichangiwa na ugumu wa maisha ya walimu ambao wamekuwa na madai ya muda mrefu.
Serikali inapaswa ijitathmini zaidi, kwamba inaposema itatoa elimu bure basi iendane na kulipa stahili za walimu ili wapate ari ya kuwa wabunifu zaidi kwa lengo la kuongeza ufundishaji utakaowezesha kupata idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu vizuri.
Tunaamini kama walimu wataangaliwa kwa kulipwa stahili zao kwa wakati, kiwango cha elimu nchini kitapanda na pia malalamiko yao ya mara kwa mara yatamalizika.
Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kusimama na wanyonge, tuna imani madai sugu ya walimu yatapatiwa ufumbuzi ndani ya kipindi kifupi na kuwawezesha kufanya kazi wakiwa na amani ya kupata stahili zao kwa wakati.
Tunaamini hata kile kiasi cha Sh124 bilioni kilicholipwa kwa walimu 182,000 katika mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi Desemba mwaka jana, haikuwa mbinu ya kuwatuliza walimu bali ni moja ya mikakati ya Serikali ya kumaliza kero hiyo iliyodumu kwa muda mrefu na kwamba mkakati huo utaendelea kumaliza deni la Sh800 bilioni ndani ya kipindi kifupi.
0 comments:
Post a Comment