MADAKTARI wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji mkubwa wa kubadilisha milango zaidi ya miwili ya moyo iliyokuwa imeziba.
Upasuaji huo umefanywa na madaktari hao kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Saifee ya Mumbai, India.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,Mkurugenzi wa Huduma ya Upasuaji JKCI, Bashir Nyangasa alisema kambi ya upasuaji ilianza Machi 26 mwaka huu na kumalizika jana.
“Tumefanya pia upasuaji wa kuvuna mishipa ya damu mguuni na kuipandikiza katika milango ya moyo iliyokuwa imeziba.
Upasuaji huu kitaalamu unaitwa ‘Coronary Artery Bypass Graft’. Tumewafanyia wagonjwa wanane,” alisema.
Alisema wamemfanyia upasuaji mtoto wa umri wa miaka minane ambaye mshipa wake mmoja ulikuwa umesinyaa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa JKCI,Dk.Peter Kisenge alisema kwa mara ya kwanza waliweza kuzibua mlango wa moyo ambao hupitisha damu isiyo na hewa ya oksijeni kuipeleka kwenye moyo, ambao ulikuwa umeziba.
“Tumewafanyia upasuaji bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa ‘cath lab’ wagonjwa 12 ambao mishipa yao iliziba kwa asilimia 100. Mgonjwa mmoja tumemuwekea betri ya pacemaker,” alisema.
Alisema tangu Januari mwaka huu hadi Machi, taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa nje ya nchi, imefanya upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 79.
“Kama wagonjwa hawa wangeenda kutibiwa nje,Serikali ingetumia Sh bilioni 2.1 na kila mmoja angegharimu zaidi ya Sh milioni 27,” alisema.
Kambi hiyo imefanyika ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani, Mtakatifu Dk. Syedna Aliqadr Mufaddal alipokutana na Rais Dk. John Magufuli Oktoba, mwaka jana.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment