Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania utakaosaidia kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi na kukabiliana na umasikini wa wananchi wa nchi zote mbili.
Mhe. Hailemariam Dessalegn ametoa kauli hiyo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili, anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Miongoni mwa maeneo ambayo Mhe. Hailemariam Dessalegn amesema atatilia mkazo ni ushirikiano katika usafiri wa anga ambapo ameahidi kuwatuma wataalamu kutoka Shirika la Ndege la Ethiopia kuja nchini kushirikiana na Wataalamu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha utendaji kazi na kuikuza ATCL.
“Shirika letu la ndege la Ethiopia ni shirika linaloendeshwa kwa faida Barani Afrika, lina ndege 96 na linatarajia kununua ndege nyingine 42, ndege zake zinatua katika viwanja 92 duniani kote na viwanja 42 ndani ya Ethiopia, hivyo nitawaleta viongozi wa shirika hili ili waje washirikiane na ATCL kuweka mkakati wa namna ya kuiendeleza ATCL na kuiwezesha kufanya kazi kwa faida” amesema Mhe. Hailemariam Dessalegn.
Pia amesema Shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL litaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuwa kituo chake cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo ya ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo jirani kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo yake duniani kote.
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Hailemariam Dessalegn ambao kabla ya kuzungumza na wananchi wamefanya mazungumzo rasmi, wamesema wamekubaliana kuwa Tanzania na Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia maji ambapo Mhe. Hailemariam Dessalegn ameahidi kuwatuma wataalamu wa nchi yake kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa kutumia maji ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kujengwa uitwao Grand Ethiopian Renaissance Dam(GERD) ambao unatarajiwa kuzalisha megawatts 6,470 za umeme.
“Mhe. Waziri Mkuu tutafurahi sana kushirikiana nanyi katika suala la uzalishaji wa nishati ya umeme kwa sababu hata sisi tunaweza kuzalisha umeme mwingi katika maporomoko ya maji ya Stiegler’s Gorge yaliyopo katika mto Rufiji” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi hao wamekubaliana kushirikianakufanya mapinduzi ya kilimo na mifugo, hasa ikizingatiwa kuwa Ethiopia inaongoza kwa idadi kubwa ya ng’ombe barani Afrika na Tanzania inashika nafasi ya pili na kwamba juhudi hizo zitakwenda sambamba na kujenga viwanda vingi vitakavyoongeza thamani ya mazao.
“Naamini kuwa tukishirikiana katika kilimo na mifugo, tutaweza kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao ikiwemo ngozi na nyama na tutatumia mashirika yetu ya ndege kuyafikia masoko mbalimbali duniani na hivyo kukuza uchumi na kuwaongezea wakulima wetu kipato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, viongozi hawa wamekubaliana kushirikiana kwa kubalishana uzoefu juu ya namna sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini na gesi, elimu na mawasiliano hususani simu.
Mhe. Rais Magufuli amesema ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Hailemariam Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, viongozi hao wameshuhudia utiaji saini wa mikataba 3 ambayo ni Mkataba wa Mkakati wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia, Mkataba wa kuanzishwa Kamisheni ya Pamoja ya Kuduma kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia.
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo asubuhi na kupokewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na akiwa uwanjani hapo amepigiwa mizinga 19, amekagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake na ameshuhudia burudani ya ngoma za asili.
Jioni hii, Mhe. Hailemariam Dessalegn atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Home
News
Slider
Serikali ya Tanzania na Ethiopia zatiliana saini ya mikataba ya ushirikiano Ikulu Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment