SERIKALI imepiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote, iwe za kidini, kimila na kiserikali bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuanzia Mei mosi, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe wakati akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro.
Alisema Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuwa na takwimu sahihi za wananchi wake iweze kupanga mipango ya kimaendeleo sambamba na kuzuia wageni kuingia kinyemela nchini.
Dk. Mwakyembe aliitaka RITA kuhakikisha inasimamia sheria ya usajili kwa sababu bila nchi kuwa na takwimu sahihi za vizazi na vifo ama ndoa, inasababisha ishindwe kusonga mbele kimaendeleo.
Alisema ndiyo maana nchi zilizoendelea zinatoa kipaumbele katika suala zima la usajili kwa wananchi wake.
“Wenzetu nchi zilizoendelea, suala la usajili wamelipa kipaumbele, sisi bado tuko nyuma, lazima tubadilike kuanzia Mei, mwaka huu,” alisema.
Akitoa mfano kwa Mkoa wa Morogoro, alisema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, mkoa huo una wakazi milioni 2.2, lakini waliosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa ni asilimia 11 tu.
Wakati huo huo, Dk. Mwakyembe ametoa onyo kwa mtendaji yeyote wa mahakama atakayelalamikiwa na wananchi kufanya kazi kinyume na maadili, ikiwamo kupokea rushwa ama kutotenda haki, kutumia mahakama kugeuza kesi za madai kuwa kesi za jinai na kutaka taarifa zote ziripotiwe kwa mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maadili.
“Kutokana na maboresho katika wizara yangu, malalamiko yote yatakayobainika yanapaswa kuwasilishwa katika kamati za mahakama zilizoundwa na wizara ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi wetu,” alisema Dk. Mwakyembe.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, wakati akitoa taarifa ya wilaya hiyo, alisema bado kumekuwapo na ushirikiano mdogo kwa watendaji wa mahakama katika ofisi yake.
Chonjo alisema kama wakishirikiana na ofisi yake, wataweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, ikiwamo utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Alisema mbali na changamoto hiyo, bado kuna kesi nyingi zanazofikishwa mahakamani zikihusu baadhi ya watu kukopeshana fedha bila ya kuwa na kibali kutoka benki.
“Kesi nyingi sasa ni watu kukopeshana fedha kiholela bila ya kuwa na kibali, katika hili tumeanza kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika,” alisema.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Vizazi na Vifo Wilaya ya Morogoro, Salma Ruhaka, alisema elimu inahitajika zaidi kwa wananchi ili kuwa na mwamko wa kujiandikisha na kutambua kuna fursa za kuwa na cheti.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment