Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Viti Maalum (CHADEMA) akiwakilisha walemavu Dkt. Elly Macha amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, Dkt Macha amefariki katika hospitali ya New Cross, Wolverhampton nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa hiyo imesema kuwa mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kuja nchini ikiwa ni pamoja na taratibu za mazishi inaendelea kufanywa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu.
Kufuatia msiba huo, Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai ameahirisha vikao vya kamati vilivyokuwa vinaendelea hadi kesho Jumamosi, Aprili Mosi, 2017.
Msemaji wa CHADEMA Tumaini Makene amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, ambapo amesema mbunge huyo alikuwa akipatiwa matibabu mkoani Arusha.
"Taarifa ni za kweli, mbunge Viti Maalum Dkt. Elly Macha amefariki, lakini sijapata bado taarifa za kina, lakini ninachojua ni kwamba amekuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu Arusha" Amesema Makene
Miongoni mwa wabunge wa kwanza kutoa taarifa za msiba huyo ni Lazaro Nyalandu ambaye kupitia mtandao wa twitter ameandika "Mbunge mwenzetu, Mhe. Dr. Elly Macha amefariki dunia leo. Wabunge wote tumeguswa sana na tukio hilo. Upumzike kwa amani dada yetu mpendwa".
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment