WANAHABARI nchini wanakusudia kumweleza Rais John Magufuli kuwa ulinzi na usalama wakati wa kutekeleza majukumu yao ni muhimu kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuelekea kilele cha siku ya habari duniani, Dar es Salaam jana, wanahabari hao walisema vitendo vinavyojitokeza katika kipindi hiki vinahatarisha maisha yao, jambo ambalo linawafanya washindwe kuwajibika ipasavyo.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo Vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tan), Salome Kitomari alisema kutokana na hali hiyo, wanahabari wanapaswa kukaa pamoja na wadau wengine ikiwamo serikali kujadili suala hilo na kulipatia ufumbuzi.
“Tunaelekea kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari itakayofanyika Mei 2 na 3 mwaka huu mkoani Mwanza.
“Katika maadhimisho hayo tutakutana na wadau mbalimbali pamoja na Rais Dk John Magufuli ambaye tutamweleza kuwa wanahabari wanahitaji ulinzi na usalama waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo,”alisema Salome.
Alisema wadau hao kwa pamoja wakiwamo wafanyakazi wa vyombo vya habari, kwenye mitandao na nje ya mitandao pia wanapaswa kutetea sera na mfumo wa mageuzi ya sheria kwa maendeleo endelevu.
Salome ambaye amepata wadhifa huo hivi karibuni alisemawanahabari pia wataweza kushirikisha wadau hao wakiwamo vijana kuonyesha na kushughulikia masuala yanayohusu kuboresha mazingira ya uwazi na uwajibikaji.
Alisema anaamini majadiliano hayo yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa pamoja wa mfumo wa sheria na udhibiti unaofaa ambao utasaidia kuboresha upatikanaji wa habari na uhuru wa kujieleza.
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inasema kuwa ‘Mawazo muhimu kwa wakati muhimu, Jukumu la vyombo vya habari, katika kuendeleza jamii zenye amani, haki jumuishi itasaidia wanahabari kutoa mawazo yao na kuangalia majukumu yaliyopo waweze kuyatekeleza ipasavyo bila ya kuwapo kwa vikwazo vyovyote.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, alisema wakati umefika kwa wanahabari kuangalia matatizo yanayowakumba waweze kuyajadili na kuyawasilishwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji.
“Tusisubiri matatizo yajitokeze ndipo tuanze kupiga kelele… tunapaswa kusema haya yaliyopo na kuyawasilisha kwenye mamlaka husika yaweze kufanyiwa kazi kabla ya athari kubwa kutokea,”alisema Makunga.
Mwakilishi wa Wakfu wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF), Razia Mwawanga, alisema mwandishi wa habari anahitaji mazingira mazuri ya kufanyia kazi aweze kutimiza majukumu yake.
Kutokana na hali hiyo wakfu hiyo imeweza kuwafadhili wanahabari kwenda katika maeneo mbalimbali kutimiza majukumu yao, jambo ambalo limechangia kuibuka changamoto mbalimbali zinazowahusu wananchi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment