Image
Image

MFUKO wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI wametoa Sh milioni 860

MFUKO wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI, jana umetoa Sh milioni 860 kwa ajili ya dawa za kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi kwa watu wanaoishi na VVU na ujenzi wa Kituo cha Afya Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amezindua namba 0684 909090 maalumu kwa ajili ya kuchangia mfuko huo.

Akizungumza kwenye kikao cha ugawaji fedha, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo, Godfrey Simbeye alisema kati ya fedha hizo, Sh milioni 660 zimepelekwa Wizara ya Afya na Sh milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mirerani.

“Kiasi kikubwa cha fedha hizo zinakwenda Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua dawa za maji na vidonge vya septrin (cotrimoxazole) ambavyo vinatumika kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi, hii ni kutokana na fedha za wafadhili kutoelekezwa katika kununua dawa hizi muhimu na pia kuziba pengo la gharama za kudhibiti Ukimwi.

“Kiasi kingine kitatumika kujenga Kituo cha Afya Mirerani na hii ni sambamba na kuunga mkono ahadi ya Rais John Magufuli ya kusaidia ujenzi wa kituo cha afya eneo hilo, ambacho kitasaidia kuboresha afya za wananchi na kutoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU,” alisema.

Lengo la Mfuko wa Ukimwi ni kuhakikisha uwepo wa rasilimali za kutosha na uhakika katika kupambana na Ukimwi kwa kuongeza ukusanyaji wa rasilimali kutoka kwa wadau wa ndani na kupunguza utegemezi wa wafadhili kwa asilimia 40.

Kulingana na Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi katika kipindi cha miaka mitano mahitaji ni Sh trilioni 6, na asilimia 93 ya hizo zinatarajiwa kutoka kwa wafadhili na asilimia 7 kutoka vyanzo vya ndani huku asilimia 56 ya fedha zote katika kipindi hicho ni kwa ajili ya ununuzi wa dawa za kufubaza VVU.

Akizungumza kabla ya kuzindua namba ya kuchangia, Jenista alisema Mfuko wa Ukimwi ni wa Watanzania wote na kuhimiza jamii kuchangia. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kuimarisha huduma za afya kwa lengo la kuwa na ustawi wa jamii, ikiwamo kundi la watu wanaoishi na VVU.

Alisema pamoja na asilimia 94.7 ya Watanzania hawajaambukizwa, wajibu wa serikali ni kuwalinda watu hao ambao ndio nguvu kazi ya nchi. “ Lengo letu ni kuwa ifikapo mwaka 2030, tusiwe na maambukizi mapya, tusiwe na vifo vinavyotokana na Ukimwi na kuondoa kabisa unyanyapaa,” alisema.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema dawa hizo zitatolewa kwa wenye VVU bure na kuwataka waganga wakuu wa mkoa kuhakikisha dawa zinafika kwenye vituo vya afya na kutumika na walengwa pekee.

Alisema kwa mwaka kiasi cha Sh bilioni 2.8 zinatumika kununua dawa za Septrin hivyo kwa kupewa Sh milioni 660, ni moja ya juhudi ya kutekeleza hilo na kuahidi kwenda kununua dawa hizo kwa watengenezaji.

Alisema pamoja na juhudi za serikali na asilimia 67 ya wenye VVU kutumia dawa za kufubaza, changamoto iliyopo ni kuwa nusu ya wanaume wenye VVU hawatumii dawa hizo, jambo ambalo linachangia kuwapo kwa maambukizi mapya.

Asilimia 76 ya wanawake na asilimia 48 ya wanaume wenye VVU ndio hutumia dawa za kufubaza. Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMSEMI), Selemani Jafo alisema utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha afya ufanyike kwa haraka huku kazi hiyo iendane na thamani ya fedha zilizotolewa
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment