Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Karimjee na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kutimiza miaka 72 tangu kuanzishwa kwake.
Makamu wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu isemayo “Maendeleo ya viwanda na utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu,” alisema umoja wa mataifa umekuwa washirika wakubwa wa maendeleo katika sekta nyingi hapa nchini hususan maeneo ya vijijini katika huduma za maji, elimu pamoja na afya.
“Umoja wa mataifa umekuwa ukifadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini, katika kutekeleza malengo yake ya millennium ya umoja huo, hivyo naomba wadau na wafadhili wa maendeleo kutoka umoja huu kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania ambayo imekuwa ikishirikiana nao kwa mafanikio makubwa na kutambua jitihada zao katika kuleta maendeleo,” alieleza Mh. Samia.Aidha alisema kuwa katika kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 serikali inatoa wito kwa wadau wote na washirika wa UN kuja kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika kujenga viwanda, vilevile aliongeza kuwa uwepo wa amani, usalama pamoja na jitihada za vita dhidi ya ubadhilifu wa rasilimali, rushwa pamoja na urasimu ni nguzo kubwa ya wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.
“Serikali chini ya Mhe. Rais Magufuli inaendelea kupambana dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya rasilimali za umma, wizi wa nyara za serikali na matumizi mabaya ya fedha za umma, serikali pia inatekeleza malengo 17 ya umoja wa mataifa kwa kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani, kuongeza makusanyo ya kodi pamoja na kuzuia mianya ya ukwepaji wa kodi,” alifafanua Makamu wa Rais.Mh.Samia aliongeza kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na UN katika harakati za kulinda amani katika mataifa mbalimbali barani Afrika kama vile Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo. Vilevile alitoa wito kwa umoja huo kufanya mabadiliko katika baraza la usalama ili kuimarisha ulinzi, amani na ushrikiano dhidi ya makundi ya kigaidi yanayozidi kuongezeka kila uchao.
Kwa upande wake Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa, UN itaendelea kushirikina na Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linapita katika mabadiliko ya kiuchumi kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
“Wakati huu ambapo Tanzania inafanya mageuzi makubwa, inapoelekea kuwa nchi ya hadi ya kipato cha kati, msaada wa UN hauna budi kuendana na mahitaji na changamoto mpya, kwahiyo hatuna budi kuchukua mwelekeo mpya katika kazi. Kupitia malengo ya maendeleo endelevu, tutahakikisha kwamba hakuna mtu hata mmoja anayeachwa nyuma,” alisisitiza Bw. Rodriguez.Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa aliongeza kuwa, kwa kushirkiana na serikali ya awamu ya tano UN watashawishi wadau na wawekezaji wengi kuja kusaidia shughuli za maendeleo ikiwemo kuwasaidia wakimbizi pamoja na kufadhili miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa viwanda, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuwawezesha na kuwalinda wanawake, watoto na vijana dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Sherehe ya kuadhimisha kuanzishwa kwa Umoja wa Matiafa imekuwa ikifanyika kila mwaka tarehe 24, Oktoba tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945 Jijini New York. Maadhimisho ya hivi karibuni yamekuwa yakitilia mkazo maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya viwanda.
Kwa sasa UN hapa nchini inatekeleza mpango uliozinduliwa hivi karibuni kwaajili ya Mkoa wa Kigoma (The Kigoma Joint Programme) ambao utatekelezwa kati ya 2016-2021 katika Wilaya tatu za Kasulu, Kibondo na Kakonko pamoja na mkakati wa maendeleo endelevu kwa ustawi wa watu na uhifadhi wa mazingira.
0 comments:
Post a Comment