Image
Image

Rais Magufuli aipongeza TANRODS kwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 4.

RAIS John Magufuli amepongeza timu ya wataalamu wa Wakala wa Barabara (TANRODS) kwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 4 kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Kyaka-Bugene mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa 59.1.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa ufunguzi wa barabara hiyo iliyogharimu Sh bilioni 81.597, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania. Alisema hatua ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia timu ya wataalamu wa Tanroads kuusimamia mradi huo wao wenyewe kwa gharama ya Sh milioni 519.2 imeokoa zaidi ya Sh bilioni 4.5 ambazo angelipewa msimamizi kutoka nje.“Napenda kuwapongeza sana Tanroads kwa kusimamia mradi huu ninyi wenyewe, zaidi ya shilingi bilioni 4 mlizookoa kwa kuwatumia wataalamu wetu kuusimamia mradi huu ni fedha nyingi sana, nataka kitengo hiki cha usimamizi wa miradi tukiimarishe, hivi sasa tunao wahandisi 15,000 wanaoweza kufanya kazi hizi, tuwatumie,” amesisitiza Rais Magufuli.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale amemweleza Rais Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene-Kasulo yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Barabara hiyo imejengwa na kampuni ya CHICO ya China. Kabla ya kufungua barabara hiyo, Rais Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth, walisafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe zilipofanyika sherehe za ufunguzi.
Aidha, akiwa njiani kuelekea Karagwe, Rais Magufuli alisimamishwa na wananchi wa Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo.
Aidha aliwataka wawasaidie wananchi kuondoa migogoro ya ardhi, kusajili mifugo yao na kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe na malighafi za kutosha kuanzisha viwanda.“Pale Mtukula tumejenga kituo cha pamoja cha huduma mpakani kati yetu na Uganda, lengo letu ni kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwa hiyo nataka kuona wananchi wa Kagera mnachangamkia fursa hii, anzisheni viwanda kama vya nyama na mazao mengine ya kilimo, fugeni mifugo kisasa ili mnufaike,” alisema Rais Magufuli.
Akiwa Bukoba Mjini kundi kubwa la wananchi wa mji huo liliusimamisha msafara wake ambapo baada ya kupokea kero mbalimbali, Rais Magufuli ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kutatua tatizo la uhaba wa maji katika mji huo na ametoa mwito kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuwasilisha serikalini andiko la kuomba kujengewa kituo cha mabasi kama wananchi walivyomuomba.“Ndugu zangu mimi nipo pamoja na nyinyi, kero zenu nazijua na tutazishughulikia, ninachowaomba punguzeni kubishana, mnapoteza muda mwingi kubishana badala ya maendeleo, mnajichelewesha, mji huu hautakiwi uwe hivi ulivyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwashukuru kwa kazi kubwa wanayofanya waandishi wa habari waliokuwa wakirekodi na kurusha matangazo ya sherehe hizo na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia, ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kyaka-Bugene zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman Sigalla King, wabunge wa mkoa wa Kagera na viongozi wa dini na siasa. Leo Rais Magufuli ataendelea na ziara yake.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment