WATU wawili wamejeruhiwa vibaya katika ajali ya basi la Nkondo lililokuwa likitokea Arusha kwenda Mwanza baada ya kugonga kichwa cha treni eneo la Karogho Relini katika Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo saa tatu usiku juzi barabara kuu iendayo Maganzo wakati basi hilo lenye namba za usajiri T 693 BUW aina ya Youtong mali ya Kampuni ya Nkondo likiendeshwa na dereva Emmanuel Warengo (34).
Kamanda alisema katika ajali hiyo, watu wawili Ramadhani Juma (38) na Eva Brown (29) walijeruhiwa kwa kuumia kifuani na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa kupata matibabu. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi kutochukua tahadhari wakati wa kuvuka barabara katika njia ya treni na alikimbia baada ya ajali hiyo na Polisi wanaendelea kumtafuta.
Katika matukio mengine, Polisi imefanya oparesheni na kuwakamata watuhumiwa 29 wa makosa mbalimbali, kati ya hao saba kwa tukio la ukataji panga kikongwe mmoja aliyepo wilayani Kishapu. Kamanda alisema katika oparesheni hiyo walikamata pikipiki saba, mifuko ya saruji 14, magodoro mawili, vifaa vya kupigia ramli chonganishi, vifaa vya kufanyia uhalifu, difu 15 za matolori, mabomba 14 ya kutengenezea pombe aina ya gongo, mashine za kuvutia maji mbili na ya kuchomelea moja.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment