Watanzania wapo katika
harakati za kumbukumbuka na hata kusherehekea muungano wa tanganyika na
zanzibar, uliokuwa umetiwa saini na Mwalimu nyerere na Abeid Amani karume 1964.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964, Zanzibar.
Ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Aprili 26,
1964, na Aprili 27, 1964 viongozi hao walikutana katika ukumbi wa Karimjee,
jijini Dar es Dalaam kubadilishana hati za Muungano.
Sheria
za Muungano ilitamka kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar zililazimika, kuwa dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar, jina ambalo lilibadilishwa Oktoba 28, 1964 na kuwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano,
sheria namba 61, ya mwaka 1964.
Msingi wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na
katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za Mwaka 1964.
Hati za Muungano zilitiwa saini na Nyerere na Karume, Aprili 22, 1964 na
hapo Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja kwa misngi inayotambulika kimataifa.
Baada ya kuungana, Mwalimu Nyerere alikuwa rais wa kwanza na Karume alikuwa
makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
![]() |
Hayati Mwalimu Nyerere ( Kushoto) na ( Kulia) ni Karume wakitia saini Hati za Muungano |
Aprili 26, 1964, bunge la Tanganyika lilipitisha sheria za Muungano, ambazo
baadayezilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
Mnamo Aprili 27, 1964 waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na
wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano Watanganyika na Zanzibar ambao ni Amani Karume, Kassim
Abdallah Hanga, Abdulrahman Babu, Hassan Nassor Moyo, Aboud Jumbe, Hasnu Makame
na Idris Abdul Wakil. Kati yao, Aboud Jumbe na Hassan Nassor Moyo wangali hai.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianisha
mambo 11 ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano ambayo ni; Katiba na Serikali
ya Muungano, Mambo ya nchi za nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya mambo
yanayohusika na hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Mikopo na Biashara za nje,
Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Kodi ya Mapato inayolipwa na watu
binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa
Tanzania unaosimamiwa na idara ya forodha, Bandari, mambo yanayohusika na
usafiri wa anga, posta na simu.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ilianisha utawala wa serikali ya mfumo wa chama
kimoja, TANU kwa Bara na ASP kwa Zanzibar. Katiba hii, ilizingatia misingi ya
makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na sheria za Muungano wa Tangayika za
Zanzibar.
Katiba hiyo ilianisha serikali mbili, uwakilishi wa Zanzibar katika bunge la
Muungano ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano na mambo yasiyo ya
Muungano kwa upande wa Tanganyika. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yahusuyo Zanzibar.
Hata hivyo mambo ya Muungano yaliongezwa kutoka 11 hadi 22 kutokana na
mahitaji ya ndani ya nchi pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yanaendelea kutokea
ulimwengini baada ya Muungano.
Mwaka 1985, jambo la 12 linalohusu sarafu na fedha kwa ajili ya malipo na
kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na benki katika Jamhuri ya Muunagno wa
Tanzania, liliingizwa.
Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, mambo matatu
ya Muungano yaliyongezwa, ambayo ni leseni za viwanda na takwimu; elimu ya juu;
na usafirishaji wa anga.
Mwaka 1968, mambo ya maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa
ya magari na ama ya petroli na aina nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia
yaliyongezwa kwenye orodha hiyo.
Aidha mambo ya
Muungano yaliendelea kuongezeka hadi kufikia 21 kufuatia kuvunjika kwa
iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya mfumo wa siasa nchini suala la 22 la
uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo
liliongezwa kwenye orodha hiyo.
KUHUSU MUUNGANO
Katika miaka hivi
karibuni kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na muundo wa Muungano,
baadhi wakitaka uwe wa zaidi ya serikali mbili, wengine serikali moja, wapo
wanaotaka Tanganyika iwe kivyake na Zanzibar kivyake.
Hata hivyo hekima inaonyesha kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unabaki
kuwa ni fahari ya Watanzania, kwani mwelekeo wa dunia katika nyanja mbalimbali,
mataifa kuungana kwa ushirikiano wa aina mbalimbali ni muhimu kuliko taifa moja
kupambana kivyake.
Urejeaji
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika mwaka 1977, uwepo wa SADC,
ECOWAS, COMESA, na jumuiya nyingine nyingi duniani kote, ni vielelezo kwamba
ushirikiano baina ya mataifa ni suala lisilohitaji mjadala.
Ieleweke kwamba hakuna ushirikiano usio kuwa na matatizo kama ilivyo kwa
Muungano wa Tanzania, vivyo hivyo muungano mwingine kama vile ya United Kingdom
(UK), Uingereza na United States of America (USA) kwa maana ya Marekani na
United Arabs Emirate (UAE), nayo ina matatizo, lakini hata mara moja mjadala
juu ya matatizo hayo siyo kuvunja ushirikiano bali kutatua na wale wanaotaka
kuvunja hushughulikiwa ipasavyo.
"Matatizo ya Muungano kama wa UK ni mabaya zaidi, na hata UAE hawana
ahueni, ila wanajua kwamba Muungano wao ni lazima. Wamarekani wanapambana na
watu wenye mawazo haya ya kuvunja miungano kwenye majimbo ya Alaska, Hawaii na
Texas na mwishowe wameamua kuweka kambi kubwa ya jeshi la nchi kavu Texas;
utitiri wa kambi za anga Alaska; na vituo vikubwa kupindukia vya majini kule
Hawaii. Hivi, hawa mabingwa wa demokrasia wanapoamua kulinda nchi yao namna
hii, unafikiri ni wajinga? Walimwaga damu na waliyanunua majimbo haya na
wamepitia shida kubwa, ndiyo maana leo wanajidai," anaandika mchangiaji
katika mjadala kuhusu Muungano.
Ni vyema Watanzania wakati huu wa kusheherekea miaka 48 ya Muungano,
kila mmoja akajisikia ufahari wa kuwa na kitu kizuri kilichoasisiwa na Waafrika
wenyewe na kudumu kwa umri huo. Mawazo ya kubaguana
kwa sababu zisizo na msingi, pengine kukidhi matakwa na wakati kama vile ya
kibinafsi na kisiasa, yasipewe nafasi kuisambaratisha nchi. Chambilecho
wahenga, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
0 comments:
Post a Comment