Na Upendo Msuya.
Serikali imesema kuwa iliamua kuidhinisha pikipiki za
matairi mawili na matatu maarufu kama bodaboda kutumika katika biashara ya
usafiri na usafirishaji wa abiria kwa lengo la kuongeza wigo wa ajira kwa
vijana kuwawezesha kupata kipato kutokana na kazi halali hivyo kuwaepusha
vijana kujiingiza katika shughuli haramu ikiwemo uhalifu.
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
ameliambia bunge mjini dodoma kuwa licha ya lengo hilo la kupanua wigo wa ajira
na kurahisisha huduma za usafiri, changamoto kubwa inayotokana na matumizi ya
pikipiki hizo ni ajali nyingi za barabarani ambazo zimegharimu maisha ya watu
wengi na kusababisha ulemavu wa kudumu jambo linalosababisha utegemezi kwa
waathirika wa ajali hizo.
Dk. Nchimbi amesema takwimu za jeshi la polisi nchini
zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari - Dec mwaka 2013 kulitokea ajali
5763 za pikipiki ambazo zimegharimu maisha ya watanzania 930, na majeruhi 5532,
ambapo mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kuwa na ajali 2,479 ambapo ajali
hizo zimesabisha vifo 164 na majeruhi 2,765 kutoka katika wilaya zote tatu,
idadi ambayo inaelezwa kuwa ni kubwa ikilinganishwa na mikoa mingine.
Kwa mujibu wa takwimu hizo mkoa wa Dar es salaam
unaongoza kwa kuwa na ajali nyingi za pikipiki ukifuatiwa na Morogoro, Arusha,
na Kilimanjaro.
Waziri Nchimbi amesema katika kukabiliana na ongezeko
hilo la ajali zinazotokana na pikipiki serikali itaendelea kutoa elimu kwa
jamii juu ya ufahamu wa sheria na taratibu za barabarani, pamoja na kuangaliwa
namna ya kuhakikisha kuwa vijana wanaoendesha pikipiki hizo wanakuwa wamepitia
mafunzo na kupata leseni kutokana na kilichobainika kwamba vijana wengi kwa
sasa hawana leseni za udereva.
0 comments:
Post a Comment