Image
Image

TAIFASTARS KUPEPETANA NA SUDAN KWENYE UWANJA WA ADDIS ABABA LEO HII NCHINI ETHIOPIA.

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha Kim Paulsen , leo inatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Addis Ababa nchini Ethiopia kupepetana na Sudan ‘Mamba wa Mto Nile’ katika mchezo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Stars itaongozwa na mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco “Abebayor” kufuatia kukosekana kwa nyota Mbwana Ally Samata na Thomas Emmanuel Ulimwengu ambao hawajajiunga na timu hiyo mpaka sasa kutokana na kuwa na majukumu ya kutumikia kibarua chao TP Mazembe katika Kombe la Shirikisho Afrika. 

John Raphael Bocco
Bila shaka John Raphael ‘Bocco’ atasimama badala ya Samatta na kipindi cha pili kocha Kim Paulsen anaweza akayahamishia majukumu ya Ulimwengu kwa Zahor Pazi au Simon Msuva, itategemea na aina ya mchezo na wapinzani. 

 Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton kujiandaa na mchezo wa Kundi C dhidi ya Morocco Juni 8 mjini Marakech kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.

Lakini kwa asilimia kikubwa kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwa kile kile kilichocheza na Morocco katika mchezo wake wa mwisho Machi 22 mjini Dar es Salaam; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa, Athumani Iddi, Frank Domayo, John Bocco na Amri Kiemba.

Kwenye benchi wanaweza kuwapo Ally Mustafa ‘Barthez’, Mwinyi Kazimoto, Mudathir Yahya, Simon Msuva, Zahor Pazi, Mwadini Ally, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Khamis Mcha, Vicent Barnabas na Haroun Chanongo.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro anatarajiwa kuwaongoza Watanzania wachache waliopo nchini humo kwenda kuishangilia Taifa Stars.

Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.

Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya Samatta na Ulimwengu kujiunga na wenzao Juni 3 mwaka huu mjini Marrakech.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment