MIZENGO PINDA - WAZIRI MKUU TANZANIA. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Ujenzi wake kugharimu sh. bilioni 6.6/-
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali
itasaidia kadri itakavyoweza kwenye ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Afya ya Mt.
Bakhita iliyopo Namanyere, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa.
Alikuwa akijibu risala ya taasisi hiyo wakati
alipoitembelea ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani
yaliyoanza jana (Jumamosi, Juni Mosi, 2013) kwenye mji mdogo wa Namanyere,
wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Ujenzi wa taasisi hiyo unaochangiwa na
wafadhili mbalimbali unatarajia kugharimu sh. Bilioni 6.6 ambapo mabweni matatu
yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 576 yanatarajiwa kujengwa. Pia madarasa manne
yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 yanatarajiwa kukamilika chini ya mradi
huo.
Maeneo mengine ni vyumba vya kujisomea,
ukarabati wa madarasa mawili ya zamani ambapo moja litatumika kama maabara ya
kufundishia na jingine litatumika kama chumba cha kompyuta kwa ajili ya
wanafunzi.
Akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu,
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sista Helena Katebera alisema taasisi hiyo
inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa fedha kwa ajili ya
uendeshaji wa shughuli za taasisi hiyo ambayo inatoa kozi ya Afya ya Uuguzi na
Ukunga pamoja na wasaidizi wa maabara zote zikiwa ni kwa ngazi ya cheti.
“Chuo kinakabiliwa na uchache wa walimu wenye
sifa stahiki; upungufu wa vitabu na vifaa vya ufundishaji kwa vitendo kwa kozi
zote mbili; ukosefu wa gari la chuo na kutolipwa madeni yanayofikia sh. milioni
80 zikiwa ni ada za wanafunzi waliodhaminiwa masomo na taasisi mbalimbali,”
alisema.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu pia alitembelea
Hospitali teule ya Wilaya ya Nkasi na kukagua baadhi ya majengo ambako pia
alielezwa kwamba uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya upanuzi wa wodi ya
wazazi ili iweze kuwahudumia wazazi tisa kwa wakati mmoja badala ya watatu kama
ilivyo sasa.
Akisoma taarifa ya hospitali hiyo mbele ya
Waziri Mkuu, Mganga Mfawidhi, Dk. Norbert Twamba alisema hospitali hiyo
inakabiliwa na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari
sita, madaktari wasaidizi 22, wauguzi 19, matabibu 10, maafisa wauguzi 13 na
wahudumu wa afya 42.
“Gari la wagonjwa limechakaa mno kwa lililopo
ni la tangu mwaka 2004 ambalo tulipewa na Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la
Sumbawanga na hadi sasa limetembea zaidi ya km.192,000,” alisema.
Vilevile, Dk. Twamba alisema hospitali hiyo
inakabiliwa na upungufu wa madawa, vifaa tiba na vitendanishi na akaomba
kusaidiwa ili waweze kutioa huduma kwa ufanisi zaidi.
Waziri Mkuu aliahidi kufuatilia maombi yao
ili kuyapatia ufumbuzi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JUNI 2, 2013.
0 comments:
Post a Comment