Janeth Jackson
anayedaiwa kula njama za kumuua mume wake, Simon Jakson na mtoto wake wa kambo.
JANETH Jackson (32), mkazi wa Moshono, Arusha na Novatus
Elias, walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya
ya Arusha /Arumeru, Devotha Kamuzora, wakisomewa makosa mawili ya kula njama ya
kutaka kumuua Simon Jackson ambaye ndiye mume wa Janeth.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Edna Kasala, alidai
mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote walitenda kosa la pili la kula njama na
kutaka kumuua Desderi Sabas, ambaye ni mtoto wa mke mwingine kwa mume
huyo anayeishi Bukoba, mkoani Kagera.
Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu
Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kasala iliomba mahakama kuwanyima dhamana washtakiwa, kwa
sababu watuhumiwa wengine wawili wanatafutwa hivyo na upelelezi haujakamilika.
Alidai kutokana na uzito wa tuhuma hizo, maombi hayo ya
kuwanyima dhamana washtakiwa yameambatana na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi
Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha.
“Mheshimiwa tunafahamu kwamba dhamana ni haki ya washtakiwa
kikatiba, lakini kutokana na mazingira ya kesi hii kuwa magumu, tunaomba
dhamana isitolewe ili kuwatafuta watuhumiwa wengine wa kesi hii,” alidai
Kasala.
Kwa upande wake,Wakili wa utetezi, Fidelis Peter, alipinga
maombi hayo na kutaka mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa kwa sababu ni haki
yao ya kikatiba na kwamba hilo ni kosa lao la kwanza.
Sababu nyingine ya kupinga maombi ya upande wa mashtaka, ni
kwamba washtakiwa wanaweza kuvuruga upepelezi wakiachiwa siyo za msingi kwani
ni watu wanaoaminika katika jamii.
“Mheshimiwa sababu za kuwanyima dhamana washtakiwa hazina
uzito wowote, pia mshtakiwa wa kwanza (Janeth) ana mtoto wa miezi sita na tangu
akamatwe alhamisi iliyopita hajamwona wala kumnyonyesha hivyo anastahili kupewa
dhamana,”alidai Wakili Peter.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili,
Hakimu Kamuzora, alikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kuamuru
watuhumiwa wapelekwe mahabusu hadi Agosti 5, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa
tena.
Katika kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi jijini hapa,
inadaiwa Janeth alitaka kumuua mumewe ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya
Tanzanite na mwanaye wa kiume, ili arithi mali na utajiri alionao
mfanyabiashara huyo.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment