Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete amewataka wanawake wa dini zote nchini kutokubaguana
kutokana na itikadi zao za vyama vya siasa bali wawe
mstari wa mbele kuhubiri amani na upendo.
Mama Kikwete
aliyasema hayo jana wakati akiwafutarisha wanawake wa dini
mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete
alisema kuwa ukosefu wa amani ukitokea katika nchi wanawake na watoto ndiyo
wahanga wakubwa hivyo basi wasikubali watu kuwadanganya
bali wawe na msimamo na umoja ili waweze kuilinda amani
ambayo ndiyo silaha pekee ya kuwaletea ukombozi iliyoasisiwa na
wazee wa nchi yao.
“Ninawashukuru
kwa kuacha shughuli zenu na kuitikia wito wangu wa kuja na kufuturu pamoja
nami, nawatakia mfungo mwema nini nyote mnaofunga ili Mwenyezi Mungu awakubalie
heri zenu nanyi msiofunga Mwenyezi Munguawabariki katika maisha yenu ya kila
siku”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania
Taifa (BAKWATA) Shamim Khan alimshukuru Mama Kikwete kwa upendo wake
wa kuwaalika wanawake hao kupata futari ya pamoja.
Mama Khan
alisema kuwa kukutana kwao kumewafanya wajifunze kuwa
wakitaka amani ni lazima washirikiane bila ya kujali rangi, dini na kabila
kwani wanawake wote wanamatatizo yanayofanana ambayo wanaweza kuyatatua kwa
pamoja bila ya kuangalia kuwa huyu ni mkristo au muislamu
na wakikaa pamoja amani inapatikana.
Naye Olive
Lwema ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wakristo Tanzania alisema kuwa
aliposikia wamepata mwaliko huo alifurahi sana kwasababu wanapokutana wanawake
ambao ni wazazi wa watoto wa taifa, wake wa waume wanaoongoza nchi hakuna jambo
litakaloharibika na ameshuhudia kwa kuona nyuso za ushirikiano na upendo baina
yao.
Mama Lwema
aliwaomba wanawake wanaofunga kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani wajitoe kufunga kwao kwa ajili ya maombi maalum ya kuombea amani na
watoto kwani hivi sasa vijana wengi wanaomaliza vyuo hawana ajira,
shule haziendi sawa na wanaopata machungu ya haya yote ni wanawake.
0 comments:
Post a Comment