IKIWA
leo ni siku ya mwisho aliyopewa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe na Jeshi la Polisi nchini kuwasilisha ushahidi wa
kuhusika kwa jeshi hilo na mlipuko wa bomu uliotokea mwezi uliopita mkoani
Arusha, kiongozi huyo amegoma kuutoa.
Jeshi la Polisi kupitia Mkurugenzi wake wa Makosa ya Jinai Julai 17 lilimwandikia Mbowe barua yenye kumbukumbu namba AR/IR/6223/2013 ikimtaka kupeleka ushahidi wake leo kabla ya saa nane mchana, kiongozi huyo amewataka polisi kumpeleka mahakamani kwani hatawapa ushahidi huo.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema kamwe hawezi kwenda kinyume cha msimamo wa chama chake walioamua kutoukabidhi ushahidi huo kwa polisi hata kama watawapa vitisho kama walivyozoea.
Alibainisha kuwa alipokea barua iliyomtaka aende polisi leo na ataitikia wito huo, lakini hatapeleka ushahidi wanaoutaka, kwakuwa wao ni watuhumiwa.
Alisema CHADEMA ilimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ikimwomba kuunda tume huru ya majaji kwa ajili ya tukio hilo, ambayo wataikabidhi ushahidi wao.
Aliongeza kuwa masuala muhimu yagusayo chama na masilahi ya taifa yanafanyika kulingana na maamuzi ya vikao, hivyo yeye hawezi kwenda kinyume cha kilichoamuliwa.
Kwa mujibu wa Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, suala la Arusha linahusisha viongozi, wanachama na wapenzi wa CHADEMA, hivyo lilifikishwa kwenye vikao na kufanyiwa uamuzi wa kutopeleka ushahidi polisi.
“Nina mambo mengi ya kukutana na polisi, nitaitikia wito wao lakini kuhusu kupeleka huo ushahidi ni msimamo wa chama kwamba hatupeleki… waende mahakamani, wachukue hatua za kisheria au waamue lolote.
“Tunasubiri kauli ya rais ya ama ataunda tume ama hataunda tume huru ya kimahakama yenye majaji. Lakini pia ninamsubiri mwanasheria wa chama ambaye anakuja kutoka Tabora, polisi nitaenda tu,” alisema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Barua ya polisi
Jeshi la Polisi kupitia Mkurugenzi wake wa Makosa ya Jinai Julai 17 lilimwandikia Mbowe barua yenye kumbukumbu namba AR/IR/6223/2013 ikimtaka kupeleka ushahidi wake Julai 23 (leo) kabla ya saa nane mchana.
“Kutokana na mahojiano uliyofanya na Polisi Mkoa wa Arusha mnamo Juni 20, 2013 kuhusu mauaji yaliyotokana na ulipuaji wa bomu huko Soweto, Arusha ulidai kuwa unao ushahidi unaobainisha wahusika wa tukio hilo.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 10 (2) na (2A) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai nchini, sura 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 202, unaamriwa kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai tarehe 23 Julai, 2013 saa nane mchana bila kukosa na ulete ushahidi huo.
“…Unatahadharishwa kuwa kushindwa au kukataa kufika na kuleta ushahidi huo ni kosa la jinai chini ya sheria iliyotajwa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hussein Laisseri, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.
Juni 15, mwaka huu wakiwa kwenye mkutano wa wazi uliokuwa ukihutubiwa na Mbowe katika viwanja vya Soweto mjini Arusha wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani wanne, bomu la kutupwa kwa mkono lililipuka na kusababisha vifo vya watu wanne na kuwajeruhi wengine 70.
Awali jeshi hilo lilituma viongozi wake wa juu mkoani Arusha kwa ajili ya uchunguzi, ambapo waliwahoji watu kadhaa akiwamo Mbowe, kwamba alisema alimwona aliyelipua bomu hilo kuwa ni askari polisi na kuweka bayana kwamba hawezi kuutoa ushahidi huo kwa polisi kwa madai kuwa watauharibu.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment