Dar es Salaam.
Serikali imetangaza viwango vipya vya chini
vya mishahara kisekta ambavyo vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine
ambavyo ni kuanzia Sh40,000 hadi Sh400,000 kwa mwezi kuanzia Julai Mosi mwaka
huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Kazi
na Ajira, Ridhiwani Wema, watakaolipwa kima kidogo zaidi cha Sh40,000 ni
wafanyakazi wa nyumbani ambao wameajiriwa na watu wa kawaida huku wakiishi
kwenye nyumba za waajiri wao.
Kwa upande mwingine, katika viwango hivyo, kima kikubwa katika
viwango hivyo cha Sh400,000 kitalipwa kwa wafanyakazi wa sekta za mawasiliano
zikiwamo kampuni za simu, kampuni za kimataifa za nishati, madini na taasisi za
fedha.
Katika viwango hivyo, mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani
walioajiriwa na watu wa kawaida lakini ambao hawaishi kwenye nyumba za waajiri
wao itakuwa Sh80,000.
“Viwango vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani
walioajiriwa na mabalozi wa kigeni na wafanyabiashara maarufu wanatakiwa
kulipwa Sh150,000 kwa mwezi,” ilisema taarifa hiyo.
Wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na maofisa wa Serikali
watalipwa Sh130,000 kwa mwezi.
Kima cha chini cha mshahara katika huduma za kilimo ni Sh100,000
na huduma za afya Sh132,000.
Kwa upande wa wafanyakazi wa vyombo vya habari, posta na usafirishaji
wa vifurushi ‘courier services’, kima cha chini kitaanzia Sh150,000.
Viwango vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa hoteli za
kitalii kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ni Sh250,000, wakati kwa hoteli za kati
ni Sh150,000 na migahawa, nyumba za wageni na baa ni Sh130,000.
Kampuni za ulinzi za kimataifa zitapaswa kulipa kiwango cha
chini cha mishahara cha Sh150,000 kwa wafanyakazi wake sawa na kampuni ndogo za
huduma za nishati. Kampuni ndogo za ulinzi zitatakiwa kulipa Sh100,000.
Kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga
kitakuwa Sh300,000, sawa na wale wa utoaji na uingizaji wa mizigo. Wafanyakazi
wanaofanya katika sekta ya usafirishaji wa majini, uvuvi na nchikavu wakitakiwa
kulipwa Sh200,000.
Kima cha chini kwa
kampuni za makandarasi daraja la kwanza kitakuwa Sh325,000, makandarasi daraja
la pili hadi la nne Sh280,000 na makandarasi daraja la tano hadi saba
Sh250,000.


0 comments:
Post a Comment