Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye
amewatahadharisha Watanzania kuwa makini na watu wanaotaka madaraka kwa kugawa
fedha katika sehemu mbalimbali za nchi au majimbo akionya wanaweza kujikuta
wakimweka madarakani kiongozi anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Hivi kama mtu anaweza kuhonga sehemu kubwa ya
wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi anayosaka
ni urais; tumeshajiuliza hizo fedha nyingi hivyo anapata wapi? Kama
anajihusisha na biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto wetu watapona?”
alisema Sumaye jana na kuongeza:
“Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea
mwaka kesho kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2015 wakati wa
Uchaguzi Mkuu.”
Alisema hayo mjini Morogoro kwenye maadhimisho ya
miaka 20 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).
Akizungumza kwa tahadhari alisema haizungumzii
Serikali yake iliyoko madarakani wala mtu yeyote, bali tabia mbaya, Sumaye
alisema biashara ya dawa za kulevya inahusisha fedha nyingi na mitandao mipana
ambayo isipodhibitiwa inaweza kulitumbukiza taifa katika janga.
Alisema Katiba Mpya siyo mwarobaini wa matatizo
yanayolikabili taifa bali, utekelezaji na usimamizi wa sheria na kwamba jambo
muhimu ni kuwa na Serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria ili kulinda yale
yaliyoelekezwa katika Katiba.
“Katiba haiwezi kumzuia mwizi kwenda kuiba na sheria
haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka adhabu ya kupewa huyo mwizi. Kwa
hiyo ili vyote hivi viwe na maana ni lazima awepo mtu au chombo cha kumkamata
huyo mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na chombo hicho ni Serikali.
Kama haiwezi kufanya hiyo kazi kwa ukamilifu tutaishia kulalamika tu na maonevu
na maumivu yataendelea kuumiza jamii.”
“Kwa hiyo hata Katiba iwe nzuri namna gani na
ikatamka kuwa rushwa ni adui wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa
hilo; kama tutaweka viongozi madarakani kwa rushwa, hiyo Katiba wala
haitatusaidia.
Hivyo Katiba nzuri mpya lazima iambatane na Serikali safi yenye
kusimamia masilahi ya umma. Huwezi kumweka madarakani mwenyekiti wa kijiji au
diwani au mbunge au hata Rais kwa rushwa ya kuwanunua wapigakura halafu
utegemee Katiba Mpya itajibu matatizo ya jamii.”
Azungumzia Mviwata
Sumaye alisema Mtandao huo wa Wakulima Wadogo
Tanzania ndiyo unaojua tatizo la kilimo na shida zao na ndiyo unaotakiwa
kuulizwa cha kufanya ili kilimo chetu kibadilike na mkulima afaidike.
“Kama hatuwahusishi na kuwashirikisha katika sera,
mipango na programu za kilimo, basi tujue kuwa sera, mipango na programu hizo
zitashindwa.”
Alisema Tanzania ni nchi ambayo wananchi wake wengi
wanategemea kilimo kwa maisha yao na uchumi wa taifa pia kwa kiasi kikubwa
hutegemea sekta hiyo, lakini bado ni duni na hakijamkomboa mkulima mwenyewe
wala uchumi wa taifa...
“Nchi na watu wake bado ni maskini pamoja na kuwa watu
wachapakazi wapo na ardhi kubwa na nzuri yenye rutuba ipo.
0 comments:
Post a Comment