Ludovick Utouh.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick
Utouh amesema taarifa ya Sh bilioni 252 zilizokuwa zimeoneshwa katika taarifa
ya Wizara ya Ujenzi, zilihamishwa kwenda Wakala wa Barabara (Tanroads) kulipia
madeni ya wakandarasi na kwamba hapakuwa na ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Utouh
alisema vyombo vya habari viliripoti suala hilo tofauti, baada ya Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC) kukutana na wizara na kuhoji juu ya matumizi ya fedha
hizo.
Utouh alisema baada ya PAC na Kamati ya Kudumu ya Serikali za
Mitaa (LAAC) kupitia ripoti ya Wizara ya Ujenzi, kumejitokeza upotoshaji wa
taarifa kuhusu hesabu za wizara hiyo na taarifa zisizo sahihi, zikidai kulikuwa
na ufisadi.
Alisema fedha hizo zimeoneshwa kwenye taarifa ya hesabu za
Wizara hiyo, kama vile ni miradi mipya ya mwaka 2011/2012 tofauti na uhalisia
wake.
Utouh alisema uhalisia wa fedha hizo ni kuwa mara baada ya
kupokewa na Wizara ya Ujenzi kutoka Hazina, zilihamishwa kwenda Tanroads
kulipia madeni ya wakandarasi wa miradi ya barabara, iliyotekelezwa na
wahandisi washauri, ambao walikuwa hawajalipwa kwenye mwaka wa fedha 2010/2011.
“Fedha hizi zilijumuishwa kimakosa kwenye hesabu za Wizara kama
matumizi ya akaunti ya maendeleo, hivyo kuongeza matumizi ya Wizara kimakosa
kwa kiasi hicho.
Kihasibu fedha hizo zilipaswa kuoneshwa kwenye hesabu za
mtumiaji halisi wa fedha ambaye ni Tanroads na siyo Wizara hiyo,” alisema
Utouh.
Alisema kutokana na hali hiyo, hesabu za wizara hazikuwa sahihi,
kutokana na uwepo wa ongezeko hilo kubwa la fedha na hivyo kusababisha kupewa
hati ya ukaguzi yenye mashaka.
“Hivyo katika kujadili hesabu za Wizara ya Ujenzi hakukuwepo na
tuhuma zozote za ufisadi, ila Kamati ya PAC ilimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali kuihakikishia matumizi ya fedha hizo, jambo ambalo
tumejiridhisha nalo kwa ushahidi wa namna mlolongo wake ulivyo hadi
zilipotumika” aliongeza Utouh.
Aidha, alisema mbali na dosari hiyo ya kihasibu, Wizara ya
Ujenzi inafanya kazi nzuri ya kusimamia na kujenga barabara katika kona zote za
nchi, hivyo viongozi wake wanapaswa kupongezwa kwa kazi hiyo wanayoifanya huku
akiwataka kuwa na moyo wa kuchapa kazi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Katika hatua nyingine, Utouh alimpongeza Spika wa Bunge Anne
Makinda kwa uamuzi wake wa kupanga upya Kamati za Kudumu ya Hesabu za Serikali
Kuu (PAC), kwa madai kuwa utasaidia kuleta ufanisi na tija katika utendaji kazi
wa kamati hiyo.
Alisema uamuzi wa Spika kuipanga upya PAC na kuwa na vyombo
viwili PAC 1, itakayokuwa ikishughulikia taarifa za Hesabu za Serikali Kuu,
idara zinazojitegemea na taasisi zingine za Serikali chini ya Mwenyekiti wake
Zitto Kabwe na PAC 11, itakayokuwa ikishughulikia hesabu za Mashirika ya Umma
chini ya uenyekiti wa Deo Filikunjombe, kutasaidia kuleta ufanisi mkubwa katika
ufuatiliaji.
Habarileo
0 comments:
Post a Comment