Sheikh Ponda Issa Ponda - Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini.
Morogoro.
Hali ya wasiwasi imetanda mjini
Morogoro bado baada ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda
Issa Ponda, kudaiwa kupigwa risasi begani wakati polisi wakiwa katika harakati
ya kumkamata.
Habari kutoka katika eneo hilo zinadai kuwa
Ponda alipigwa risasi saa 12:25 jioni, wakati akisindikizwa na wafuasi wake
kuelekea katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja, baada ya kumaliza kutoa
mhadhara katika kongamano lilifanyika mjini Morogoro jana.
Tukio hilo lilitokea katika Barabara ya
Tumbaku, baada ya kumalizika kwa mkutano wa kongamano lililoandaliwa na Jumuiya
ya Wahadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro.
Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa
Msema aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa Ponda alipigwa risasi sehemu ya
bega, na askari polisi na kwamba aliwahishwa kutibiwa katika Hospitali ya
Kiislamu iliyopo eneo Msamvu mjini Morogoro.
Hata hivyo, wakati Sheikh huyo akisema hivyo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alikanusha madai ya kuwa
polisi wamempiga risasi.
Alisema polisi walifika katika eneo hilo kwa
ajili ya kumkamata Ponda, baada ya kumaliza mhadhara wake na kwamba wakati
wakitaka kumkamata ndipo wafuasi wake wakawazuia polisi na kulazimika kupiga
mabomu ya machozi na risasi hewani kuwatawanya.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa Sheikh Ponda
aliyekuwa katika gari ndogo huku wafuasi wake wakimsindikiza kwa miguu,
walipofika eneo la gereji mabomu ya machozi yalipigwa na polisi waliokuwa
katika magari aina ya defender wakati wakijaribu kuwatawanya wafuasi hao.
Baada ya tukio hilo baadhi ya wafuasi wake
walimchukua Sheikh Ponda kutoka katika gari lake na kumkimbizia katika gereji
moja, kisha wakatoka wakiwa wamempakia katika pikipiki na kumpeleka katika
Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Mlinzi mmoja wa lango namba moja alisema kuwa
ulifika msululu wa pikipiki zaidi ya 50, lakini pikipiki zote zilizuiliwa
isipokuwa iliyokuwa imembeba Sheikh Ponda na kwenda naye mpaka mapokezi.
Aidha, alisema wakiwa katika eneo hilo magari
kadhaa ya polisi yaliingia katika lango la hospitali hiyo. Hivyo wafuasi wa
Sheikh Ponda wakalazimika kumbeba begani na kutoroka naye kupitia lango namba
mbili.
Taarifa zilizopatikana baadaye zinadaiwa kuwa
Sheikh Ponda alikimbizwa katika Hospitali ya Kiislamu ya Msamvu.
Baadhi ya watu walidai kumwona Sheikh Ponda
akiingizwa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro, lakini walishangaa alivyotoweka.
0 comments:
Post a Comment