Dk. Wilbrod Slaa
Chama cha Demokrasia na
Maendeleo CHADEMA kimekosoa mfumo wa elimu nchini kwamba haulengi kuwafanya
wahitimu kuwa wabunifu wanaoweza kukabiliana na changamoto za ajira, hatua
ambayo imesababisha tatizo la vijana wasio na ajira kuongezeka kila mwaka.
Akifungua kongamano la
uchumi na ajira Tanzania lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chama hicho
BAVICHA, Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Wilbrod Slaa amesema mfumo wa elimu
uliopo unawafanya wahitimu kutegemea ajira ya kuajiwa serikalini pekee.
Amesema hata vyuo vya
elimu ya ufundi kwa maana ya veta bado vimeshindwa kukabiliana na mazingira
halisi ya kuwafanya wahitimu wa vyuo hivyo kubuni namna ya kujiajiri, jambo
ambalo ni changamoto kwa vyuo hivyo kushindwa kufikia malengo ya kuanzishwa
kwake.
Dk. Slaa amesema ni
jukumu la vijana wenyewe kufikia maamuzi magumu ya kufanya mabadiliko ili
kuondokana na hali hiyo, kwani vinginevyo wataendelea kubaki katika giza, na
matokeo yake ni kujitumbukiza kwenye vitendo viovu hususan vya kuvuta bangi na
kutumia madawa ya kulevya.
Slaaa pia
alizungumzia namna serikali inavyokosa kubuni masuala ya kipaumbele katika
kuimarisha uchumi, kwa kutenga fedha kwa miradi isiyotoa tija kwa wananchi,
akitolea mfano wa mabilioni ya JK zilizokusudiwa kwenda kwa wakulima na
wajasiriamali lakini zikaishia kwa wajanja wachache wa mijini.
Kongamano hilo, pamoja
na mambo mengine linakusanya mawazo na maoni ya vijana wa chama hicho juu ya
changamoto zinazowakabili vijana wa Tanzania ili mawazo hayo yaunganishwe
katika kutengeneza sera za chama hicho kwa ajili ya uchaguzi ujao.
0 comments:
Post a Comment