MADIWANI wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) waliofukuzwa katika Manispaa ya Bukoba, wamesema wako tayari
kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kama chama chao
kitaendelea na msimamo wa kuwafukuza. Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya
simu, mmoja wa madiwani hao (jina na kata yake tumevihifadhi), alisema wako
tayari kuhamia Chadema muda wowote kama hawatarudishiwa uanachama wao.
Alisema, madiwani wote
waliofukuzwa wana msimamo mmoja, ambapo wanasubiri vikao vya Kamati Kuu ya CC
ili wajue hatima yao, lakini vikishindwa kuwarudisha kwenye chama, watahamia
Chadema ili kuendeleza harakati zao walizozianzisha.
Alisema, wanachokifanya wao
ni kutetea maslahi ya taifa na wananchi waliowapigia kura na si kulinda
biashara za watu binafsi, hata kama wanaungwa mkono na uongozi wa juu wa CCM.
Msimamo huo wa madiwani
umekuja siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kuwakaribisha
madiwani hao katika chama chake na kusema wako tayari kuwafundisha siasa za
mageuzi.
Mbowe aliyasema hayo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru, mjini Bukoba, juzi,
katika mwendelezo wa mikutano ya mabaraza ya wazi ya chama hicho kujadili rasmu
ya Katiba mpya.
Mbowe alikwenda mbali zaidi
akisema chama chake kiko tayari kushirikiana na kiongozi wa CCM anayepinga
ufisadi kama anavyofanya Mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki.
Alipoulizwa kama wamepata
mawazo ya kujiunga na Chadema, baada ya kauli ya Mbowe, diwani huyo alisema wao
walikwishakuwa na mawazo hayo, lakini kauli ya mwenyekiti huyo imewaweka huru
zaidi.
“Si kama tumeamua sasa,
mawazo ya kuhamia Chadema tulikuwa nayo baada ya uongozi wa mkoa kutangaza
kutuvua uanachama, lakini kwa kauli ya Mbowe kutukaribisha rasmi, kumetujengea
ari mpya kwamba hatujapotea.
“Tatizo letu na meya
linafahamika kwamba ni ufisadi wake tulioulalamikia tangu mwaka jana, kwenye
vikao vya Baraza la Madiwani, hatukusikilizwa, badala yake tunaonekana wasaliti
wa chama.
“CCM wanapaswa kujua kwamba,
hoja za wapinzani zikiwa sahihi wananchi wanawaunga mkono, vivyo hivyo na sisi
hatuwezi kubeza hoja zao kwa sababu tu ni wapinzani, tutaonekana watu wa
ajabu,” alisema diwani huyo.
“Tumefarijika na kauli ya
Mbowe, baadhi yetu tulikuwepo katika mkutano wake jana (juzi) pale Uwanja wa
Uhuru, ni suala la muda tu mtasikia Bukoba imezaliwa upya,” alisema.
Mbali na hilo, mgogoro huo
unaofukuta katika Halmashauri ya Bukoba unahusishwa na sababu za kisiasa kati
ya Kagasheki na Meya wa mji huo, Anatory Amani.
Balozi Kagasheki, ambaye pia
ni Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), anatajwa kuwa na uhasama wa kisiasa na kada
mwenzake, Amani, ambaye awali wawili hao walikuwa na ushirika wa karibu.
Madiwani wanane waliofukuzwa
wanatuhumiwa kushirikiana na wenzao wa upinzani kusaini hati maalum na
kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige
kura ya kumng’oa madarakani Meya Amani mwishoni mwa mwaka.
Kikao cha Halmashauri Kuu ya
CCM Mkoa kilichokaa Agosti 3, mwaka huu, kiliwafukuza uanachama na uongozi
madiwani hao, akiwamo Mwenyekiti wake wa Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na
Diwani wa Kata ya Kashai.
Wengine waliofukuzwa mbali na
mwenyekiti huyo, ni Diwani wa Kata ya Buhembe, Alexander Ngalinda, ambaye pia
ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Wengine na kata zao kwenye
mabano ni Meya wa zamani wa manispaa ya hiyo, Samwel Ruhangisa (Kitendaguro),
Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Deus Mutakyahwa (Nyanga).
Wengine ni Robert Katunzi
(Hamugembe), Richard Gasper (Miembeni) na Murungi Badru Kichwabuta, Diwani wa
Viti Maalumu.
MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment