TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili na kutolea
maamuzi pamoja na mambo mengine suala la Madiwani wanane waliotangazwa
kufukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera.
Katika maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha uamuzi uliofanywa
na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013 wa kuwafukuza
uanachama Madiwani hao. Hivyo Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri
Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012
Ibara ya 93 (15). Ibara hiyo inasomeka kuwa moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya
CCM Mkoa ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi
wake wa mwisho unafanywa na
Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua
uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa
maelekezo”.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya Madiwani wa CCM wa Manispaa ya
Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu,
mshikamano na amani katika Manispaa na Chama.
Kamati Kuu pia imeitaka Serikali kufanya ukaguzi wa haraka wa
mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na hatua stahiki
zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza Serikali za Mitaa.
Wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya zikichunguzwa; Kamati Kuu
inawataka Madiwani wa CCM kurejesha utulivu kwenye Manispaa na Chama kwa
ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea
maendeleo wananchi wa Bukoba.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM
ITIKADI NA UENEZI
27/08/2013
Nape Moses Nnauye
CCM Secretary for Ideology & Publicity
0 comments:
Post a Comment