DODOMA.
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema
baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja
hadharani kwa haraka.
Majibu
hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya wabunge kumbana na wengine wakizomea
baada ya kueleza ugumu wa kutaja majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa
kutosha.
“Serikali
haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa
mahakamani,
hivyo lazima tuwe makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni
fulani wakati hatuna vithibitisho.
“Kumbukeni
wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha
hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine
inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi alipokuwa akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse.
Katika
swali lake ambalo lilisababisha kelele za kuzomea, Natse alitaka majina hayo
yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne
Makinda kuingilia kati na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani,
acheni tabia hiyo lazima mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini
mtindo huu si mzuri...”
Patashika
hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige
aliyetaka kujua iwapo Serikali inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara
hiyo nchini na kama haioni kama kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo
katika viwanja vya ndege na juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.
Akijibu
swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa
na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu
kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.
Alisema
Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo la matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa
za kulevya nchini na alitaja takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi
cha kuanzia mwaka 2000 hadi Machi, 2012.
Alisema
pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa
mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa
Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.
Hata
hivyo, katika swali lake la nyongeza, Magige alisema uteketezaji wa dawa
zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa siri kiasi cha kutiliwa shaka kuwa huenda
zinachukuliwa na maofisa waliozikamata ndiyo maana hakuna uwazi.
Kuhusu
hilo, Waziri Lukuvi alisema suala la uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi
kutokana na sheria zilizopo kutotoa nafasi ya kuteketezwa mapema kwa kuwa
zinatumika kwa ajili ya ushahidi akisema wakati mwingine hukaa zaidi ya miaka
10.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment