Dk. Ali Mohamed Shein.
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amefanya
mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kupangua idara zilizokuwa zikisimamiwa na
wizara mbalimbali na kuunda wizara mpya nne.
Taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya
Mzee, katika mabadiliko hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kubakia na Wizara 16 kama ilivyokuwa zamani.
Taarifa hiyo imetaja Wizara mpya zilizoanzishwa
ni Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais tawala za mikoa na Idara maalum za SMZ ambayo
Waziri wake atakuwa Haji Omar Kheir, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na
Utawala Bora itakayoongozwa na Dk. Mwinyihaji Makame.
Wizara nyingine ni Ofisi ya Rais Kazi na
Utumishi wa Umma, itakayoongozwa na Haroun Ali Suleiman na Wizara ya Fedha
ambayo itakuwa chini ya Omar Yusuph Mzee.
Katika mabadiliko hayo idara
zilizohamishwa kutoka Wizara moja kwenda nyingine ni idara ya uwezeshaji ambayo
imehamishiwa katika Wizara ya Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ambayo
itaongozwa na Waziri Zainab Omar Mohamed.
Idara nyingine ni utumishi wa umma
na utawala bora na kuhamishiwa katika ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, shughuli za tume ya mipango zimehamishiwa ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi kutoka Wizara ya Fedha na idara ya uratibu wa
shughuli za SMZ Dar es Salaam zimehamishiwa ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Aidha, Dk. Shein amefanya uteuzi wa Makatibu
Wakuu na Naibu Makatibu wakuu katika Wizara hizo mpya na mabadiliko hayo ameyafanya
kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
0 comments:
Post a Comment