KATIKA kile
kinachoweza kutafsiriwa kama wabunge wa kambi ya upinzani wameondoka na muswada
wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, CCM
wameshindwa kujadili hoja na kujikita kuwakejeli na kuwatusi wenzao.
Hatua hiyo
ilijitokeza jana jioni baada ya Bunge kurejea kwenye mjadala wa muswada huo,
lakini wabunge takriban wote 12 wa CCM waliopata nafasi ya kuchangia walishind
wa kujikita kwenye
hoja.
Pamoja na wabunge
hao kukiuka kanuni kwa kujadili mambo yaliyo nje ya mjadala, naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai, alishindwa kuwakemea badala yake alikuwa akishangilia kwa
kuchomeka maneno ya kuwasifia.
Wabunge hao
waliopata nafasi ya kuchangia majimbo yao kwenye mabano ni Masauni Yusufu
Masauni (Kikwajuni), Mary Mwanjelwa (Viti Maalum), Khamis Kigwangalah (Nzega),
Paul Lwanji (Manyoni).
Wengine ni Kombo
Khamis (Tumbe), Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba (Mbinga Magharibi),
Stella Manyanya (Viti Maalum), Richard Ndassa (Sumve), Saidi Nkumba (Sikonge),
Adam Malima (Mkuranga) na Erasto Zambi (Mbozi Mashariki).
Wabunge hao kwa
nyakati tofauti walitumia muda wao kuwajadili wabunge wa CHADEMA na CUF huku
wengine wakisahau kabisa kugusia hata muswada wenywewe.
Mapema asubuhi,
ngumi matusi na maneno ya kejeli vilitawala ndani na nje ya ukumbi wa Bunge
baada ya askari wa Bunge kujaribu kumtoa nje kiongozi wa kambi rasmi ya
upinzani, Freeman Mbowe, bila mafanikio.
Hali ilivyokuwa
Hali ya machafuko
ndani ya Bunge ilitokana na baadhi ya wabunge wa vyama vyote kuomba mwongozo wa
Spika kwa ajili ya kumtaka aondoe majadiliano ya muswada huo.
Wabunge hao walidai
muswada huo ulikuwa haujakidhi mahitaji ya utoaji maoni hususan kwa upande wa
Zanzibar.
Miongozo hiyo ilimfanya
Naibu Spika, Job Ndugai, kukubali hoja ya kupigwa kura ya kuwahoji wabunge
wanaotaka muswada huo uondolewe.
Hata hivyo, mbunge
wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) alimtaka Spika kuruhusu upigwaji wa kura za
mtu mmoja mmoja badala ya kutumia kura jumla ya ndiyo au siyo.
Ndugai alikubaliana
na Mnyika na kuruhusu kupigwa kura kwa kuwaita majina wabunge na wale waliosema
ndiyo walimaanisha muswada uondolewe na wale waliosema siyo walimaanisha
uendelee.
Alibainisha kuwa
wabunge waliotakiwa kupiga kura ni 351 ambapo 136 hawakuwepo na waliopiga kura
ya siyo walikuwa 156 na ndiyo 59.
Ndugai alisema
waliokuwa wakitaka hoja hiyo iondolewe wameshindwa hivyo alianza kumpa nafasi
mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) kuchangia.
Hata hivyo kabla ya
Mrema kuzungumza Mbowe alisimama kuomba mwongozo wa kiti lakini Ndugai alikataa
na kumtaka aketi chini na hivyo kumruhusu Mrema aendelee.
Hatua ya Mbowe
kunyimwa nafasi wakati kanuni za Bunge zinaruhusu kiongozi huyo kupewa nafasi
wakati wowote anaposimama, iliwafanya wapinzani kusimama wote kumpinga Ndugai.
Ndugai katika
kujihami kibabe alipoona hali hiyo, aliwaomba askari wa Bunge kujiandaa kwa
dakika tano na kama mambo hayatatulia atawaruhusu waingie ndani ya ukumbi wa
Bunge.
Baada ya hali
kutotulia, Ndugai aliwaita askari waingie ukumbini ili wamtoe nje Mbowe jambo
lililozidisha tafrani kwa wabunge wenzake kumkinga asiguswe.
Mbunge wa Mbeya,
Joseph Mbilinyi, Silvester Kasulumbayi (Maswa Mashariki), Moses Machali (Kasulu
Mjini) waliwaongoza wenzao kuwazuia askari wasitekeleze agizo la Ndugai.
Askari hao
walilazimika kusubiri kwa muda usiopungua dakika tano huku wakifanya
majadiliano na wapinzani juu ya kumtoa nje Mbowe.
Wakati hali hiyo
ikiendelea, Ndugai alikuwa amesimama kwenye kiti chake huku akizuia vipaza
sauti vya wabunge visifanye kazi ili matusi na kejeli visisikike.
“Askari hamjaja
hapa ndani kwa majadiliano nataka mara moja mwondoeni kiongozi wa kambi ya
upinzani na ni lazima aondoke ndani ya ukumbi huu,” alisisitiza.
Askari hao
walilazimika kumwondoa mzobemzobe Mbilinyi huku wakimkwida na kumwangusha
chini.
Wakati Mbilinyi
akitolewa nje, Kasulumbayi aliwadhibiti askari waliokuwa wakitaka kumuondoa
Mbowe barabara wakashindwa kumtoa.
Wabunge wengine
John Mnyika (Ubungo), Machali (Kasulu Mjini) na Moza Abeid wa CUF Viti Maalum,
walizongwa na askari hao ambao mmoja wao alimvua hijabu mbunge huyo.
Baada ya vurugu
kuwa kubwa zaidi ya dakika 30, Mbowe aliamua kutoka mwenyewe ndani ya ukumbi
akifuatwa na wabunge wengine wote wa vyama vya upinzani vya CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi huku Mrema wa TLP akibaki na CCM.
Nje ya Bunge
Hali ilizidi kuwa
tete nje ya Bunge, ambapo wapinzani walikuwa wakiwatuhumu askari kwa kukubali
kuwa sehemu ya CCM.
“Usalama ni
CCM…usalama ni CCM, usalama hautoinusuru CCM, 2015 tuwanawang’oa CCM…usalama
mtaenda wapi?” walihoji.
Wakiwa nje ya
viwanja vya Bunge, askari waliongezwa wakiwa kwenye magari mbalimbali ambapo
walimuomba Mbowe aingie kwenye gari ili hali itulie.
Hata hivyo,
Mbilinyi aliamua kumvaa mmoja wa askari aliyemtuhumu kumpiga wakati akimtoa
ndani ya Bunge.
Vurugu hizo
zilipungua baada ya Mbowe kuamua kuingia kwenye gari lake na kuwataka wabunge
wenzake wamuingize Mbilinyi kwenye gari hilo pia.
Ndugai ababaika
Baada ya wapinzani
kutoka nje, Ndugai alisema kuwa hakuna adhabu yoyote itakayowakabili wabunge
hao.
Alijitetea kuwa
kanuni inayompa nafasi kiongozi wa upinzani kusimama wakati wowote ni muda wa
maswali kwa waziri mkuu na baada ya hapo busara ya kiutu tu ndiyo inatumika na
si haki yake.
Ndugai alisema kuwa
alimpa nafasi Mrema badala ya Mbowe kwa vile naye ana haki ya kuzungumza,
kwamba kitendo alichokifanya kiongozi huyo wa kambi ya upinzani ni ubinafsi.
Mbatia, Lissu
wachachamaa
Wabunge wa upinzani
hawakuingia kwenye kikao cha jioni badala yake walikutana na kuweka msimamo wa
pamoja wakimlaani Ndugai kwa kitendo chake cha kumdhalilisha Mbowe.
Katika mkutano huo
wasemaji wakuu walikuwa ni Mbowe (CHADEMA), Habib Mnyaa (CUF) na James Mbatia
(NCCR-Mageuzi).
Akizungumzia
kitendo hicho, Tundu Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, alisema
kitendo cha Ndugai kutompa nafasi Mbowe ni tukio la kuandaliwa.
“Wanadhani
wamemdhalilisha Mbowe…si kweli bali wamelidhalilisha Bunge na kiti cha Spika
ambacho sasa kinaonekana hakijui au hakisimamii kanuni za mabunge ya Jumuiya ya
Madola, kanuni hizo zinawatambua viongozi watatu bungeni,” alisema.
Lissu aliwataja
watu wanaotambulika kuwa ni Spika, Kiongozi wa Shughuli za Serikali na Kiongozi
wa Upinzani ambao mmoja wao akisimama basi mbunge yeyote anatakiwa kukaa chini
ili atoe hoja aliyonayo.
Aliongeza kuwa
kitendo cha kusema hotuba ya upinzani ni ya uongo si cha kweli kwani
Wazanzibari hawakushirikishwa ingawa Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah aliruhusu
Kamati ya Katiba na Sheria kwenda visiwani Zanzibar kupata maoni hayo.
Naye Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema CCM ndiyo itakayoifanya nchi isitawalike
wala si wapinzani kama inavyodaiwa.
Mnyaa kwa upande
wake alisema kuanzia sasa ni mwanzo mzuri kwa vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na
CHADEMA kuunganisha nguvu zao kupambana na CCM au wale wote wasioitakia mema
Tanzania.
‘Tutaungana katika
masuala yote muhimu, hatuna ugomvi kwenye maslahi ya taifa, lakini kadiri
tunavyokwenda tutapunguza uadui,” alisema.
Mbowe naye alisema
angependa kuona tofauti na vyama vya upinzani zinazidi kupungua.
“CCM wasitarajie wakipitisha
sheria hii ndio itakuwa Katiba mpya, ngoma iko kwa wananchi wasitarajie jambo
hili ni jepesi, wangoje waone huko mitaani kuna nini,” alisema.
TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment