DODOMA.
JANA, Bingwa wa Dunia wa uzani wa
kati (super middle), unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF),
Francis Cheka alitembelea Bunge baada ya kutwaa taji hilo karibuni na jana
hiyohiyo, Bunge hilo lilishuh
udia ngumi kavukavu katika vurugu
kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukumbi wake.
Katika masumbwi hayo yasiyo
rasmi, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anadaiwa kumpiga
kichwa Askari wa Bunge na kumchania sare na kung’oa kipaza sauti.
Mbilinyi jana alisema alikuwa
anatafutwa na polisi huku akisema hilo limemshangaza akidai kwamba yeye ndiye
aliyeshambuliwa na askari huyo.
Vurugu hizo zilitokea baada ya
Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Katika vurugu hizo Mbilinyi
alibebwa juujuu na polisi hadi nje ya ukumbi huku akiwa hana viatu.
Pamoja na tafrani hiyo, Ndugai
alisema wakati akihitimisha kikao cha Bunge kipindi cha asubuhi kuwa
amewasamehe wabunge wote waliohusika na kosa hilo la utovu wa nidhamu na
kuwaruhusu kurejea kipindi cha jioni kuendelea na Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo, wabunge wote CUF,
NCCR-Mageuzi na Chadema ambao baada ya tukio hilo walitoka nje ya ukumbi,
hawakurejea na baadaye walitoa msimamo wa pamoja wakisema hawatashiriki katika mjadala
huo.
Msimamo huo ulitolewa na Mbowe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
na Mbunge wa CUF, Habib Mnyaa.
Mbowe alisema wameamua kususia
majadiliano hayo kuonyesha msimamo wao wa kupinga kupitisha mambo yasiyo na
masilahi kwa nchi.
“Hatuko tayari kushiriki katika
uchakachuaji wa Katiba... Matumizi ya nguvu ya polisi kamwe hayatatupatia
Katiba nzuri,” alisema. Alisema kambi rasmi ya upinzani inalaani vikali kitendo
cha Ndugai kuruhusu Bunge kunajisiwa kwa kuruhusu polisi kuingia ndani kinyume
na kanuni.
Mnyaa alisema kitendo cha wadau
wa Zanzibar kutoshirikishwa katika kutoa maoni yao katika muswada huo wa
marekebisho ni dharau kubwa.
Mbatia alisema Tanzania haiwezi
kuingia Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa kwa sababu tayari kuna
mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Tundu Lissu alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi kutoa ushahidi kama Rais aliteua wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kulingana na mapendekezo ya taasisi zao.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment