Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa
pamoja na Mmiliki wa Hoteli ya Sun Set Bungalows iliyoko katika Kijiji cha
Kendwa Nungwi Abdulsamad Ahmed Said akikagua athari iliyosababishwa na moto
mkubwa uliyoyakumba baadhi ya majengo ya Hoteli hiyo juzi jioni.
Pembeni
yao aliyevaa kofia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A”
Machano Fadhil Machano { Babla } na Nyuma yao aliyevaa suti za Bahari ni
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk.
Na Othman Khamis Ame, OMPR.
Baadhi ya Majengo ya Hoteli ya
White Sand iliyopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika Kijiji cha Kendwa
Nungwi ikiwa ni miongoni mwa majengo 10 ya hoteli hiyo yaliyoteketea kwa moto
mapaa yake juzi jioni. Picha na Hassan Issa wa OMPR – ZNZ.
Hasara ya zaidi ya Shilingi
Bilioni Moja Nukta 2 imepatikana kufuatia kuungua kwa moto hoteli mbili za
Kitalii za White Sand na Sun Set Bungalows ziliopo katika Kijiji cha
Kendwa Nungwi Wilaya ya Kaskazini “ A” Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi majira ya
saa 11.00 za jioni.
Hoteli ya Sun Set Bungalows
inakadiriwa kupata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni mia 400,000,000/- wakati
ile ya White Sand iliyoungua zaidi kutokana na moto huo inakadiriwa
hasara ya zaidi ya shilingi Milioni mia 800,000,000/-.
Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja Pembe Juma Khamis akimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif hali halisi ya moto ulivyoikumba
Hoteli ya White Sand iliyoko Kendwa Nungwi Mkoani humo juzi jioni.
Moto huo ulisababishwa na
hitilafu za umeme katika moja ya majengo ya Hoteli ya Sun Set Bungalows
iliyoezekwa makuti na kutoa cheche za moto zilizosambaa kwa haraka katika
baadhi ya majengo mengine kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma katika
eneo hilo.
Makamu wa pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitokea Bungeni Mjini Dodoma alifika eneo
hilo la tokeo ili kuwafariji Wamiliki, Wafanyakazi wa Hoteli hizo pamoja na
Wananachi wanaozizunguuka Hoteli hizo kutokana na maafa hayo makubwa kwa uchumi
wa Taifa.
Akitoa ufafanuzi wa mkasa
halizi wa tukio hilo Mmiliki wa Hoteli ya Sun Set Bungalows Abdullsamad
Ahmed Said alimueleza Balozi Seif kwamba Moto huo umevikumba vyumba Vinane vya
kulala wageni, Stoo pamoja na jiko la kupikia.
Abdullsamad alisema Wageni
wapatao sabini waliokuwemo kwenye vyumba vya Hoteli hiyo waliweza kuokolewa kwa
ushirikiano kati ya Wafanyakazi wa Hoteli hiyo na Wananchi walioizunguuka
Hoteli hiyo jambo ambalo lilileta faraja kwa Uongozi pamoja na wafanyakazi
wake.
Mmiliki huyo wa Hoteli ya Sun Set
Bungalows aliwashukuru wananchi hao, Viongozi wa Serikali Wilaya na Mkoa wa
Kaskazini Unguja pamoja na Maafisa wa Kamisheni ya Utalii kwa msaada wao
ulichangia kupunguza machungu ya janga hilo.
Balozi Seif Ali Iddi akikagua hali
ya tukio la moto huo ambao pia uliathiri Hoteli nyengine ya jirani ya
White Sand ambapo Mmoja miongoni mwa Viongozi wa Hoteli hiyo Ramadhan
Msanif alimfahamisha Balozi Seif kwamba wakati wakijiandaa kutoa
msaada kwa wenzao jirani wa Sun Set cheche za moto huo pia zikaanza kuvamia
Hoteli yao na kulazimika kukabiliana nalo.
Bwana Msanif alisema licha
ya juhudi walizochukua kukabiliana na moto huo lakini kasi kubwa ya upepo
uliokuwa ukivuma wakati huo ulisababisha kuathiri mapaa ya nyumba
10 za hoteli hiyo katika kipindi kifupi kwa vile zilikuwa na mapaa ya
makuti.
Akizungumza na Viongozi,
Wafanyakazi wa Hoateli hizo pamoja na Wananchi wa jirani na Hoteli hizo Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi
kuendelea kusaidia wawekezaji wakati yanapotokea majanga kwenye maeneo ya
vitega uchumi.
Balozi Seif alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar bado inasisitiza na kutegemea sekta ya Utalii ambayo kwa
sasa inasaidia kuongeza mapato ya Taifa sambamba na kutoa ajira kwa wananachi
wanaovizunguuka vitega uchumi hivyo.
Hata Hivyo Balozi Seif aliendelea
kuwakumbusha wawekezaji vitega uchumi mbali mbali Nchini kujenga utamaduni wa
kuiwekeza Bima Miradi yao ili wakati wanapopatwa na majanga au maafa Bima hizo
ziweze kuwasaidia.
Alisema inasikitisha kuona ipo
miradi ya kiwango kikubwa cha fedha inayoendelea kuwekezwa Nchini lakini
wamiliki wengi wa miradi hiyo wanashinda kuikatia bima na hatiame inakufa
kabisa pale inapokumbwa na majanga kama ya moto.
“ Wawekezaji na hata Wafanyabiasharawengi
bado wamekuwa wazito kuiwekea Bima miradi yao na kusahau kwa kuona
ghali mpango huo ambao kumbe huwa unawasaidia wakati wanapopatwa na
majanga “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliwapongeza Wananchi waliopo jirani na Hoteli hizo kwa juhudi kubwa
waliyochukuwa na kusababisha kupungua kwa hasara kubwa iliyokuwa
izikumbe hoteli hizo.
Alisema juhudi hizo
zilizowaongezea nguvu za uokozi wafanyakazi wa hoteli hizo zimesaidia kuokoa
mali na vifaa vya hoteli pamoja na wageni waliokuwa wakipata huduma ndani ya
Hoteli hizo.
“ Nafarajika kusikia kwamba
harakati za uokozi wa mali na vifaa katika Hoteli hizi mbili za White Sand na
Sun Set Bungalows za Kendwa hakukuwa na ripoti za udokozi wa mali kama
zilivyotokea Kwenye Hoteli ya Paradise Beach Resort iliyopo Marumbi
wakati ilipowaka moto wiki moja na nusu iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliushauri Uongozi wa Hoteli hizo kufikiria kubadilika katika
mfumo wa ujenzi wa mapaa ya makuti ili kujilinda na majanga yanayoweza
kuepukwa licha ya kwamba mfumo huo hutoa ajira kwa wananchi wanaouza makuti
yao.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliangalia eneo lililopembezoni mwa Bara bara
mbele ya Skuli ya Msingi na Sekondari ya Mto Pepo ambalo liko katika hali mbaya
kimazingira.
Ziara hiyo ya ghafla ya Balozi
Seif ilikuja kufuatia baadhi ya wananchi kufanya Biashara katika eneo hilo
linalotishia afya za Binaadamu kutokana na kutuwama kwa maji machafu yanayoweza
kusababisha maradhi ya kuambukiza.
Katika kulitafutia ufumbuzi
tatizo hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuagiza Sheha wa Shehia ya
Mto Pepo pamoja na Diwani wa Wadi ya eneo hilo kufika Ofisini kwake Vuga
Jumatatu ya Tarehe 9 Septemba asubuhi kulijadili suala hilo.
Hali ya mazingira ya eneo
hilo mbali ya kutoa sura mbaya kwa wapita njia na wageni lakini pia
inaweza kusababisha mripuko wa maradhi hasa kwa wanafunzi wadogo
wasiozingatia afya zao wa Skuli ya jirani na eneo hilo.http://www.zanzinews.com
0 comments:
Post a Comment