Nilinyanyuka kwenye kochi la nyumbani kwangu nikiwa
mzito na kwenda kulala moja kwa moja ikiwa ni mapema sana kuliko kawaida yangu.
Hii ilikuwa baada ya kuangalia timu yangu niipendayo ikadhalilishwa katika
dimba la Etihad usiku wa jumapili ya wiki iliyopita.
Nilijiuliza swali moja tu
hivi ni kweli hata kuna ushindani mkubwa msimu huu kama inavyosemekana baina ya
vilabu viwili vya jiji la Manchester.
Vilabu vyote viwili vinajinasibu kwamba vipo katika
muda wa mapito baada ya kubadilisha makocha, lakini ushindi wa 4-1 wa City
dhidi ya majirani zao ulionyesha utofauti mkubwa uliopo baina ya vikosi vya
klabu hizi mbili.
City wana ukamilifu kwenye idara, ubora wa ufundi, na
matamanio ya dhati ya kurudisha ubingwa wa Premier League chini ya kocha mwenye
ufundi mkubwa hasa kwenye mechi kubwa kama hizi.
Katika michezo mitano ya ligi ambayo tayari Man United
tumeshacheza, inaonekana wazi inabidi tubadilike sana au tusihau kuhusu ubingwa
na kuweka kipaumbele katika kumaliza ndani ya TOP 4.
David Moyes alipewa ratiba ngumu - na hata akalalamika
kuhusu ratiba hiyo ngumu - lakini mscotish huyu amepata pointi moja tu katika
michezo yote mitatu tuliyocheza na timu kubwa zenye upinzani nasi katika ligi
na kikosi chake kimecheza kwa kiwango cha kuridhisha kwenye mchezo mmoja tu wa
ligi.
Ukiachana na mchezo wa kufungua ligi dhidi ya Swansea,
United tumekuwa tukionekana kukosa ubora wa pamoja kama timu, huku safu yetu ya
ulinzi ikiyumba hasa kwa viwango vya wachezaji wetu wenye umri mkubwa kiasi
kama Rio Ferdinand na Patrice Evra.
Ujio wa Marouane Fellaini katika siku ya mwisho ya
usajili ulikuwa muhimu sana, lakini United bado wana tatizo sana katika safu ya
kiungo - hawana uimara wa kuweza kufananisha na safu ya kiungo cha Chelsea,
City, Tottenham, na sasa hata Arsenal wanaoringia ujio wa 'The Master of
Assists' Mesut Ozil na mkabaji Matheiu Flamini.
Kitu kingine cha kuhuzunisha ni upangaji wa kikosi wa
kocha, inaonekana bado anafanya majaribio wakati wapinzani wetu wengine
wanaogombea TOP 4 wakiwa wameanza vizuri ligi, pamoja na kwamba wamebadilisha
makocha na wengine hata wakiwa wameuza wachezaji mategemeo katika msimu
uliopita.
United sasa kwa bahati nzuri tuna mechi ambazo angalau
unaweza kuziita nyepesi mpaka pale tutakapokutana na 'The inform Gunners'
Arsenal November 10.
Lakini angalau hizi mechi na timu ndogo tusifanye makosa
au Moyes ajiandae kutuletea aibu ya kukosa ubingwa na kukosa hata kushiriki
Champions League msimu unaokuja.
Chanzo:Shaffihdauda
0 comments:
Post a Comment