Tanzania imesema ongezeko la bei ya pembe za ndovu
huko Mashariki ya Mbali, umaskini wa wananchi na tamaa ya baadhi ya watu ni
baadhi ya vichocheo vikubwa kwa ujangili wa tembo nchini humo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki
amesema hayo katika mahojiano maalum na Idhaa New York, Marekani ambako yuko
kwa ajili ya kushiriki mkutano wa ngazi ya juu ya nchi za Afrika na Umoja wa
Mataifa kuhusu udhibiti wa ujangili wa ndovu.
Amesema mambo hayo yalifanya hali ya ujangili wa tembo
kuwa mbaya lakini kwa miezi minane iliyopita hali imeanza kuimarika kutokana na
hatua zinazochukuliwa za kuthibiti vitendo hivyo na hata kukamatwa kwa baadhi
ya shehena za meno ya ndovu.
Balozi Kagasheki amesema kinachofanyika sasa ni
kuimarisha hatua za udhibiti ili kuondokana na kukamata shehena hizo pekee na
badala yake kuzuia kabisa ujangili wa tembo na tayari mazungumzo ya hivi
karibuni kati ya Rais Jakaya Kikwete na ujumbe wa Marekani huko Washington DC
yalikuwa mazuri kwani kuna miradi itakayofadhiliwa na Marekani.
0 comments:
Post a Comment