Reginald Mengi.
MWENYEKITI Mtendaji
wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, wameingia katika mzozo mzito kuhusu uwekezaji katika sekta ya
gesi.
Katika mzozo huo,
Mengi amemshambulia Waziri Muhongo kwa kumwita ni mwongo, mpotosh
aji na mwenye lengo
la kuwatoa Watanzania kwenye hoja ya msingi ya rasilimali yao ya gesi.
Mengi alitoa kauli
hiyo jana kupitia taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari
mbalimbali nchini.
Mzozo wa vigogo hao
ulianza wiki mbili zilizopita baada ya Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa
taasisi ya Uwekezaji nchini (TPSF), kukutana na waandishi wa habari na kueleza
msimamo wa taasisi hiyo katika suala la uwekezaji wa gesi nchini.
Katika maoni yake,
TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi
na kuishauri serikali kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi hadi sera ya gesi
itakapokuwa tayari na taasisi hiyo iliomba kukutana na Waziri Muhongo kwa
majadiliano zaidi.
Baada ya ushauri
huo, Waziri Muhongo alijibu kupitia vyombo vya habari kwamba mpango wa kugawa
vitalu vya gesi na kuingia mikataba uko palepale kama ulivyopangwa kufanyika
Oktoba mwaka huu.
Prof. Muhongo pia
alitamka bila kumng’unya maneno kwamba hana mpango wa kukutana na TPSF, kwani
kufanya hivyo ni kupoteza muda, na kuongeza kuwa uwezo wa wafanyabiashara wa
Tanzania ni kuwekeza kwenye soda na juisi, si kwenye sekta ya gesi.
‘CCM Tanzania’ kama
anavyojiita, alidai katika barua pepe yake kuwa Mengi amepanga kuwatumia vijana
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya kongamano lenye maudhui:
‘Rasilimali za nchi na manufaa kwa wazalendo.’
Alisema kongamano
hilo limepangwa kupewa muda maalumu na Kituo cha Televisheni cha ITV
kinachomilikiwa na Mengi na lengo lake ni kutaka kuionesha jamii kuwa Waziri
Muhongo na watendaji wengine wa wizara hiyo hawajali masilahi ya wazawa na
hawana utaifa wala uzalendo.
‘CCM Tanzania’
alisema si mara ya kwanza kwa sekeseke la aina hii kuzuka ama kuzushwa chini ya
uratibu na usimamizi wa Mengi na mara zote amekuwa akitumia nguvu ya ushawishi
wa vyombo vya habari anavyovimiliki katika kutafuta kuungwa mkono na hata
kuonesha ubaya wa wabaya wake.
Akijibu tuhuma hizo
kupitia taarifa yake jana, Mengi alisema Septemba 7, mwaka huu, alipokea barua
pepe yenye kichwa cha habari kisemacho: “Ubinafsi/ufisadi wa Mengi na chuki/
fitna kwenye maendeleo.”
Alisema aliyetuma
barua pepe hiyo ambayo Tanzania Daima ina nakala yake, alijitambulisha kama
‘CCM Tanzania’ na aliisambaza kwa vyombo mbalimbali vya habari, wanasiasa na
watu wengine wa kada mbalimbali.
“Kabla ya barua
pepe hiyo, nilifowadiwa pia nakala ya ujumbe (sms) na watu ambao walitumiwa na
Prof. Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na mbunge inayosema:
“Wambieni
Watanzania: Kampuni za Mengi zimeshikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa
mita za mraba 3,752.37 (sq km) amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza.
Watanzania wanakosa mapato na ajira! Sasa anataka vitalu vya gesi na mafuta.
Je, huu ndio uzawa?
“Mengi hana uzawa
bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali wa vitalu vya rasilimali zetu. Waelezeni
Watanzania ukweli huu,” alisema.
Mengi katika
taarifa yake hiyo, aliendelea kusema kuwa mbali ya Waziri Muhongo kutuma ujumbe
huo, vilevile Septemba 5, alijibu kwa dharau swali la mwandishi wa habari
lililouliza:
“Waziri tunataka
ufafanuzi kuhusu kauli yako ya hivi karibuni kwamba Watanzania hawana uwezo wa
kuwekeza katika uwekezaji wa gesi asilia.
Kwanza, kauli hii
ni kweli? Pili, kauli kwamba Watanzania wanaweza kuwekeza kwenye sekta ya
machungwa tu, huoni si kwamba unawavunja moyo bali unawadhalilisha wawekezaji
wazalendo?”
Alisema kuwa Prof.
Muhongo alijibu: “Kila mtu alitoa mawazo ya sera ya gesi wakiwamo TPSF. Mengi
na wenzake wanataka vitalu wafanye ulanguzi wa gesi na mafuta yetu. Tutatoa
orodha ya vitalu vya madini vilivyoko mikononi mwa Mengi ambavyo anafanya
ulanguzi. Ukweli utaonyesha ubabaishaji na ulanguzi wa Mengi wa genge lake.”
Mengi alisema
ameona ni bora atumie haki yake ya kujibu na kuwaonya wanaohusika kusambaza
taarifa hizo kuchafua jina lake, wajue kwamba atawachukulia hatua za kisheria.
Kuhusu kusingiziwa
kwa vitalu vya madini katika hoja ya gesi, alisema huo ni upotoshaji na uongo
wa hali ya juu wa Waziri Muhongo, wenye lengo la kuwatoa Watanzania kwenye hoja
ya msingi ya rasilimali yao ya gesi, kwani hajawahi kufanya udalali kwenye
vitalu vya madini.
Alisema tamko la
TPSF, lilitokana na kikao cha bodi ya taasisi hiyo cha Agosti 28 na baadaye
kufanya mkutano na waandishi wa habari.
Alisema mambo mengi
yalizungumzwa katika kikao hicho, ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa Watanzania
(Economic Empowerment) na mambo muhimu matatu yalijadiliwa na kutolewa
mapendekezo.
Mengi aliyataja
mambo hayo kuwa ni kuhusu manunuzi ya umma (public procurement), ardhi na uvuvi
na tatu, ni suala la gesi asilia.
“Kwenye mkutano na
waandishi wa habari, mimi nikiwa Mwenyekiti wa TPSF, niliwasilisha maoni ya
TPSF kuhusiana na manunuzi ya umma, wakati Makamu Mwenyekiti wangu, Salum
Shamte, aliwasilisha maoni yetu kuhusiana na sekta ya ardhi na uvuvi na
mwishoni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliwasilisha maoni ya
TPSF kuhusiana na gesi asilia.
“Katika maoni yetu,
TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi
na kushauri kusitishwa ugawaji wa vitalu vya gesi hadi hapo sera ya gesi
itakapokuwa tayari.
Mwisho, Bwana
Simbeye alisema kwamba TPSF itaomba kukutana na Profesa Muhongo kuwasilisha mawazo
na mapendekezo ya taasisi hiyo,” alisema.
Kwa mujibu wa
Mengi, matokeo yake Prof. Muhongo hajajibu hoja na badala yake alitoa majibu ya
kumshambulia mwenyekiti huyo.
“Binafsi
nilishitushwa na msimamo wa Prof. Muhongo, kwani Serikali ya Awamu ya Nne imepiga
hatua kubwa katika kudhihirisha kuwa ni “serikali sikivu”. Ingemgharimu nini
Prof. Muhongo kukaa na kutusikiliza? Hakuna ambacho angepoteza zaidi ya dakika
chache za muda wake.
“Jambo la pili
ambalo lilitokea ni mimi binafsi kushambuliwa kana kwamba maoni yaliyotolewa
kuhusiana na gesi ni maoni yangu binafsi na si ya TPSF. Mifano ya mashambulizi
dhidi yangu ni kama nilivyoonyesha hapo juu katika email na ujumbe mfupi wa
simu (sms),” alisema.
Msimamo wa Muhongo
Katika taarifa
hiyo, Mengi alishangazwa na undumila kuwili wa Prof. Muhongo katika suala la
uwekezaji wa gesi.
Alisema, mara baada
ya Muhongo kuingia wizarani alisema kinaga ubaga kwamba sheria iliyopo haikidhi
mahitaji ya sekta ya gesi asilia ndiyo maana akasimamisha ugawaji wa vitalu vya
gesi na kuamrisha mikataba ipitiwe upya na sera ipatikane.
“Leo tunashuhudia
Prof. Muhongo akila matapishi yake na kusema kwamba sheria zile zile
alizoziponda sasa zinafaa,” alisema.
Alisema msimamo wa
Prof. Muhongo kuhusu uwekezaji wa gesi mara baada ya kuteuliwa kuwa waziri
ulikuwa ni kutaka kupitishwa kwanza kwa sera ya gesi asilia kabla ya kuendelea
na ugawaji wa vitalu vya gesi.
Alisema hii
imejionesha katika kauli ya Muhongo Septemba 2012 ambapo alikaririwa akisema: “Baadhi
ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa.” Na “Sitovumilia mikataba ambayo
haina masilahi kwa nchi na inawanufaisha wachache.”
Baada ya hapo,
Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha ugawaji wa vitalu vya
gesi ambao ulipangwa kufanyika Septemba 2012 na kupitia upya mikataba yote.
Kwa mujibu wa
Mengi, baada ya kauli hii ya Waziri Muhungo, zoezi la kugawa vitalu vya gesi
asilia lilisitishwa lakini hadi sasa matokeo ya kupitia upya mikataba
hayajatolewa hadharani.
Alisema miezi michache
baadaye, Februari 26, 2013, Profesa Muhongo alisisitiza msimamo wake wa kutaka
Tanzania kuwa na sera ya gesi kabla ya kugawa vitalu zaidi.
Aliyasema hayo
alipokuwa akihutubia mkutano uliofanyika Chatham House, mjini London. Mkutano
huo ulipewa jina “Tanzania: An Emerging Energy Producer”.
Mengi alisema jambo
la kushangaza, Profesa Muhongo amebadilika na sasa anataka vitalu vigawiwe
kabla ya kuwapo kwa sera ya gesi.
Alisema Prof.
Muhongo amenukuliwa na gazeti la Daily News la Agosti 31, 2013 akieleza sababu
zake za kutaka vitalu vigawanywe kabla ya kupitishwa kwa sera ya gesi ambazo
hazina mashiko.
“Sababu kuu
alizozisema Muhongo kubadili msimamo wake ni tatu; mosi, ushindani wa soko na
majirani zetu, akitolea mfano wa Msumbiji. Pili, sheria ya mwaka 1960
iliyoanzisha TPDC na Sheria ya Petroli ya mwaka 1980, kwamba zinatosha
kusimamia ugawaji wa vitalu, akimaanisha sera na sheria mpya zitafuata baada ya
ugawaji wa vitalu; na tatu, Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika sekta
hii akimaanisha waachiwe wageni peke yao,” alisema Mengi.
Alisema kauli ya
Prof. Muhongo kwamba wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza tu kushiriki biashara
ya juisi na soda na hawana uwezo wa kushiriki katika biashara ya gesi yao ni
dharau.
“Kigezo gani
Profesa Muhongo anatumia kutoa kauli ya jumla yenye kutawaliwa na hisia?
Amefanya utafiti gani kupima uwezo wa kifedha wa wafanyabiashara wa Kitanzania?
Kwa taarifa yake, wapo wafanyabiashara wengi ambao wanaweza kupata fedha kwa
ajili ya kuchimba visima vya gesi,” alisema Mengi.
Akijibu barua pepe
ya mtu aliyejiita ‘CCM Tanzania’, aliyesema Mengi si mzalendo, Mwenyekiti huyo
alisema Watanzania ndio wanaojua uzalendo wake.
“Ningependa kupuuza
tuhuma kwamba mimi si mzalendo Wantanzania wanafahamu ukweli. Vilevile
ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi ni mbinafsi na sipendi maendeleo ya
Watanzania wenzangu kwa hili pia Watanzania wanafahamu ukweli,” alisema.
Alisisitiza kuwa
hapingi uwepo wa wawekezaje wageni katika sekta ya gesi lakini kuna mambo
mawili anapigania; mosi, Watanzania wanufaike na rasilimali yao ya gesi na
pili, iwepo sera ya gesi inayotoa kipaumbele kwa Watanzania.
Mimi napenda maendeleo ya nchi
yangu; kwa hiyo hata siku moja siwezi kupinga uwekezaji ama ubia na wawekezaji.
Ninachosimamia ni manufaa kwa nchi yangu.
TANZANIA DAIMA.



0 comments:
Post a Comment