DAR ES SALAAM NA ZENJIBARI.
WAKATI Rais Jakaya Kikwete
akisubiriwa asaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa
2013 ili kuwa sheria kamili, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamemshauri asifanye hivyo,
wakisema itapatikana Katiba Mpya isiyo na tija.
Wananchi hao kutoka Tanzania Bara
na Zanzibar walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Rais Kikwete anatakiwa kutumia
busara ya kushauriana na kupata maoni ya watu wa kada mbalimbali ili kujua nini
kifanyike, kabla ya kuamua kusaini muswada huo.
Mjadala wa muswada huo
uliopitishwa Ijumaa iliyopita na wabunge wengi wakiwa wa CCM, ulizua tafrani
bungeni iliyosababisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) kutolewa nje na askari.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya
wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote
wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Wapinzani walisema Serikali
iliubadili kwa nguvu muswada huo kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia
walilalamikia kitendo cha wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya
Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni ya upande huo wa muungano.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Gaudence Mpangala alisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya
ulikuwa ukienda vizuri... “Lakini umebadilika vibaya, tena katika kipindi
muhimu.
Kupitishwa kwa muswada na kusubiri saini ya Rais kunaweza kuleta Katiba
Mpya, ikawa siyo ile ambayo Watanzania wanaitarajia.” Alishauri busara itumike
kabla ya kusainiwa kuwa sheria kamili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu
Zanzibar, Ali Uki alisema hakuna haja ya muswada kukimbiliwa kusainiwa kwani
katiba ni mali ya wananchi na kuupitisha ili uwe sheria bila kuyashirikisha
makundi mengine, kutaendeleza malalamiko na kurudisha nyuma malengo ya
kupatikana kwake.
Uki alisema upo wasiwasi kwamba Katiba Mpya itatokana na
utashi wa kisiasa badala ya matakwa ya wananchi, jambo ambalo alisema linaweza
kuathiri malengo ya kuandikwa kwake.
“Utashi wa vyama umeanza
kujitokeza, huku chama kimoja kikiwa na uwakilishi mkubwa kwenye Bunge hilo,
chama kimoja kina uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge la Katiba,” alisema
Uki.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu
kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo kwamba vina kasoro kwa kuruhusu wabunge wa
Bunge la Katiba kufanya uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu
wa theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Profesa mwingine wa UDSM, Chris
Peter Maina alisema ikiwa kuna nia njema ya kupata Katiba bora, lazima suala la
uwiano wa idadi ya wabunge katika Bunge la Katiba litazamwe upya.
“Rasimu ya pili ikishatolewa na
kukabidhiwa kwa Bunge la Katiba, kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo
itakuwa imekwisha. Sasa inakuwaje Bunge linajadili Rasimu ya Katiba huku
waliyoiandaa hawapo, hiki kitu kinashangaza,” alisema Profesa Maina.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Frank
Tilly alisema hakuna umuhimu wa kukimbiza muswada kutiwa saini wakati kuna
mambo mengi ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi... “Watanzania
hawajakubaliana kwa pamoja, ili jambo liwe zuri ni lazima pande mbili au zaidi
zenye masilahi na kitu husika zikubaliane, sasa hilo halijafanyika tunakimbilia
wapi?” alihoji.
MWANANCHI


0 comments:
Post a Comment