Image
Image

RAIS OBAMA KUSITISHA KWA MUDA KUISHAMBULIA SYRIA.

Rais wa Marekani Barack Obama amekubali kusitisha kwa muda mpango wa kuishambulia kijeshi Syria, baada ya utawala wa rais Bashar al-Assad kukubaliana na pendekezo la kukusanya na kuharibu silaha zake za kemikali.

Katika hotuba yake aliyoitoa akiwa katika iluku ya White House, Obama alisema amewaomba wabunge kuchelewesha kura ya kuamua iwapo waruhusu hatua za kijeshi dhidi ya Syria, wakati Marekani ikitathmini mpango wa Urusi.

Rais Obama alisema ataendela kuwasiliana binafsi na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin, na atamtuma waziri wake wa mambo ya kigeni John Kerry kwenda mjini Geneva kwa mazungumzo leo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov. 

"Ni mapema mno kusema iwapo mpango huu utafanaikiwa, na makubaliano yoyote laazima yahakikishe kuwa utawala wa Assad unasimamia ahadi zake. 

Lakini mpango huu unaweza kuondoa kitisho cha silaha za kemikali bila matumizi ya nguvu, hasa kwa sababu Urusi ni mmoja wa washirika wakubwa zaidi wa Assad," alisema rais Obama.

Mtu ambaye hakutambuliwa akifuatilia hotuba ya rais Obama, kuhusu ushiriki wa Marekani nchini Syria. 

Mashambulizi bado yako palepale.

Obama alisema meli za marekani zinazobeba makombora ya masafa marefu zitaendela kuwepo mashariki mwa Mediterrannean, tayari kushambulia, akisisitiza kuwa hata mashambulizi yenye kikomo yatatuma ujumbe kwa kwa Assad ambao hakuna taifa lingine linaweza kuwasilisha.

Tofauti na hapo nyuma ambapo maafisa wa serikali walikuwa wanazungumzia uwezekano wa mashambulizi mnamo muda wa siku chache, hotuba ya Obama ilijielekeza zaidi upande wa diplomasia.

 Lakini alisitiza kuwa lazima zikuchuliwe hatua kwa sababu:"Tukishindwa kuchukua hatua, utawala wa Assad hautaona sababu ya kuacha kutumia silaha za kemikali, na wakati marufuku ya kutumia silaha hizi inapofutika, madikteta wengine hawatafikiria mara mbili kupata gesi ya sumu na kuitumia."

Syria yahaha kujinasua.

Wakati huo huo, Syria imeahidi kusalimisha silaha zake za kemikali, ikiitikia wito uliotolewa na mshirika wake Urusi, kwamba silaha zake ziwekwe chini ya udhibiti wa jumuiya ya kimataifa, na imesema kuwa itasaini mkataba wa Umoja wa Mataifa unaopiga marufuku matumizi ya silaha za kemikali.

Waziri wa mambo ya kigeni Walid al-Muallem aliliambia shirika la habari la Urusi Interfax, kuwa wako tayari kueleza wapi zilipo silaha hizo, kusitisha utengenezaji wake na kuonyesha viwanda vyake kwa wawakilishi wa Urusi na mataifa mengine. 

Syria ni moja ya mataifa saba wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambayo hayasaini mkataba wa mwaka 1993 unaopiga marufuku matumizi ya silaha za kemikali.

Ripoti za vyombo vya habari zinasema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria,Muallim huenda akakutana na waziri mwenzake wa Marekani John Kerry mjini Geneva. 

Rais Putin, mshirika wa Assad mwenye nguvu zaidi, alisema mapendekezo hayo yanaweza kukomesha mgorogoro, pale Marekani itakapoondoa kitisho cha mashambulizi.

Ufaransa nayo yasema adhabu iko palepale.

Washirika wa Marekani, Uingereza na Ufaransa walisema wanaandaa mswaada wa azimio kali la Umoja wa Mataifa litakaloruhusu matumizi ya nguvu, iwapo Syria itashindwa kusalimisha silaha zake. 

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius, alisema mswaada huo wa azimio hilo utapendekeza adhabu kubwa ikiwa Syria itakiuka wajibu wake, huku waziri mkuu wa Uingereza David Cameron akisema mswaada huu utakuwa na ratiba kali za utekelezaji.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema siku ya Jumatano kuwa nchi yake inaendelea na dhamira yake ya kuiadhibu Syria kutokana na matumizi ya silaha hizo, licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea. 

Hollande aliyasema hayo katika mkutano na mawaziri wake wa ulinzi na mambo ya nje pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi, uliolenga kupanga hatua zinazofuata katika mgogoro huo.

Naye rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso alisema hatua kali zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali, na kuitaka serikali mjini Damascus, kuonyesha utayari wake wa kuharibu silaha pasipo kuchelewa. 

Akiwasilisha hotuba yake ya kila mwaka kwa bunge la Umoja wa Ulaya, Barosso alisema matumizi ya silaha za kemikali ni kitendo cha uovu kinachopaswa kulaaniwa na kupata jawabu zito.

Uhalifu wa kivita waongezeka.
 
Huku haya yakijiri, wachunguzi wa haki za binaadamu wa Umoja wa mataifa, wamesema katika ripoti yao iliyotolewa Jumatano, kuwa vikosi vya serikali ya Syria viliwachinja raia, kurilipuwa hospitali na kutenda uhalifu mwingine wa kivita katika mashambulizi ya kurejesha maeneo yaliyokuwa mikononi mwa waasi mwaka huu. 

Wamesema wapiganaji waasi pia, wakiwemo wapiganaji wa kigeni wa jihadi, walitenda uhalifu wa kivita, yakiwemo mauaji, utekaji nyara na kushambulia maeneo ya raia.

"Wanaotenda uhalifu huu na ukiukaji katika pande zote, wanafanya hivyo katika ukiukaji wa sheria ya kimataifa, hawaogopi kuwajibishwa, kwa hivyo ni muhimu kuwaelekeza katika mkondo wa sheria," ilisema taarifa ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mtaifa inayoongozwa na Paulo Pinheiro kutoka Brazil.

Mgogoro wa Syria ulianza baada ya vikosi vya Assad kufanya ukandamizaji mbaya dhidi ya maandamano ya kuipinga serikali mwezi Machi 2011, na kugeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimewaua watu zaidi ya 100,000.
 DW
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment