Wenyeviti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi),
leo wanatarajia kukutana na wahariri na waandishi wa habari kueleza mikakati na
mbinu watakazozitumia kunusuru taifa lisiingie kwenye utungaji wa Katiba mpya
itakayobeba masilahi ya chama tawala.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa mikutano ya
hadhara, maandamano na elimu kwa umma juu ya athari ya muswada huo ni miongoni
mwa mbinu zitakazotumiwa kuhakikisha Rais Kikwete hasaini muswada huo au
serikali inapeleka tena mabadiliko ya sheria hiyo katika Bunge lijalo iwapo
rais atasaini.
Wapinzani wanadai kuwa serikali iliubadili kwa nguvu muswada
huo kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo cha wajumbe wa
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni
ya upande huo wa muungano.
Wakati wapinzani wakijipanga kuweka wazi mikakati ya
kumshinikiza Rais Kikwete asisaini muswada huo, wadau mbalimbali wamemtaka
kiongozi huyo atumie busara ili taifa lipate katiba itakayokuwa na manufaa kwa
taifa kuliko inavyoonekana itikadi za vyama kugubika mchakato huo.
Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Mbowe alikionya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kuwa wasitarajie kuwa kupitishwa kwa marekebisho ya muswada
huo ndiyo Katiba mpya, bali kura ya maoni ndiyo itakayoamua jambo hilo.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa wapinzani
wamejipanga kuhakikisha wananchi wanaitumia kura ya maoni kupinga mpango wa
Rais Kikwete na serikali yake kupitisha Katiba mpya yenye mwelekeo wa kukibeba
chama tawala.
Hoja za wapingaji
Kamati Maalumu ya Katiba, nayo imepinga marekebisho ya
muswada huo ikiainisha eneo mojawapo lenye tatizo ni kuruhusu asilimia 72 ya
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kubeba wanasiasa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Khoti Kamanga, alisema iwapo
Katiba mpya itaundwa bila upungufu unaoonekana sasa kupatiwa ufumbuzi
itazalisha migogoro zaidi, itakayosababisha nchi kuingia kwenye machafuko.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5 cha
muswada huo kwamba vina kasoro, kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la Katiba kufanya
uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu wa theluthi mbili kutoka
Zanzibar na Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, naye anapinga
muswada huo kwa madai kuwa una upungufu mkubwa, ukiwamo wa Zanzibar
kutoshirikishwa, pia kumpa nafasi kubwa rais kuteua watu kutoka katika asasi
mbalimbali badala ya watu hao kuteuliwa moja kwa moja na asasi au asasi husika.
Hofu ya yaliyotokea
Kenya
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza
Tanzania Daima Jumapili kuwa Tanzania inafuata njia iliyopitwa na Kenya katika
kupata katiba mpya, ambayo ilipatikana baada ya kutokea machafuko mwaka 2007
mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Mwaka 2005, wananchi wa Kenya wakiongozwa na wanasiasa
maarufu, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka, waliibwaga serikali ya rais mstaafu
wa nchi hiyo, Mwai Kibaki, katika kura ya maoni ya kuamua kuikubali au kuikataa
rasimu ya katiba iliyokuwa imependekezwa na utawala wa rais Kibaki.
Ni kutokana na matokeo ya kura hiyo, uchaguzi mkuu wa 2007
ulizaa machafuko na mauaji ya mamia ya Wakenya wasiokuwa na hatia, baada ya
kushindikana kupatikana kwa katiba mpya, hivyo utawala wa Kibaki kuamua
kuitisha uchaguzi mkuu kwa kutumia katiba na sheria za uchaguzi za zamani
zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu.
Wachambuzi wa siasa hapa nchini wanasema kuwa mwenendo wa
hivi karibuni wa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Tanzania unaonesha ishara
za wazi za kutokea yaliyotokea nchini Kenya. Kwamba, kushindwa kufikia mwafaka
baina ya wabunge wa Bunge la Tanzania lililomaliza vikao vyake hivi karibuni
mjini Dodoma, kuhusu muundo wa Bunge Maalumu la Katiba ni uthibitisho wa wazi
wa matatizo yanayoweza kutokea siku za usoni.
Bunge Maalumu la Katiba ndilo litakaloandaa rasimu ya mwisho
ya Katiba mpya itakayopelekwa kwa wananchi mapema mwakani kwa ajili ya kura ya
uamuzi, hivyo muundo wake na kukubalika kwake ni jambo muhimu na linalohitaji
mwafaka wa kitaifa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA
ilipeleka mapendekezo ya kutaka uwakilishi wa Bunge hilo upanuliwe kutoka
wajumbe 600 wa sasa na kuwa wajumbe 789 ili kulifanya bunge hilo lisihodhiwe na
wanasiasa ambao zaidi ya asilimia 70 ni wanachama wa CCM.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilishindwa baada ya wabunge wa
CCM kutumia wingi wao katika Bunge hilo kuyakwamisha mapendekezo ya upinzani na
badala yake kuamua kuendelea na muundo wa sasa unaoipa CCM haki ya kisheria ya
kulihodhi Bunge la Katiba.
Wachambuzi hao wanatabiri kuwa kama Rais Jakaya Kikwete
atakubaliana na msimamo wa wabunge wa chama chake, kwa kuitia saini sheria ya
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba na hatimaye kuwa na Bunge la
Katiba na baadaye kura ya maoni, basi kuna uwezekano katiba hiyo mpya
ikakataliwa na wananchi katika kura ya maoni kama ilivyokuwa kwa Kenya mwaka
2005.
Kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya 2011, kama
wananchi wataikataa katiba inayopendekezwa, basi katiba ya zamani itaendelea
kutumika katika shughuli zote za nchi, ikiwamo kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015, jambo ambalo linapingwa vikali na viongozi, wanachama, wafuasi wa vyama
vya upinzani na wanaharakati.
Ni kutokana na mazingira haya wachambuzi wa masuala ya siasa
nchini wanaamini na kutabiri kuzuka kwa ghasia, machafuko na umwagikaji wa damu
kama ilivyotokea Kenya mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Alli, anasema: “Tunakabiliwa na hatari mbele
yetu, maana tunakwenda kwenye kura ya maoni kuhusu Katiba mpya tukiwa
tumemeguka vipande vipande. Tulipaswa kufika huko tukiwa wamoja kama taifa,
tulipaswa kuwa na mwafaka wa kitaifa katika suala hili la katiba ya nchi badala
ya kwenda kwa kuongozwa na itikadi zetu za kisiasa,” alieleza Bashiru na
kuongeza:
“Machafuko na mauaji yaliyotokea Kenya baada ya uchaguzi
mkuu wa 2007 yalitokana na makosa ya utawala wa rais mstaafu wa nchi hiyo, Mwai
Kibaki, ambaye aliamua kuwadharau na kuwapuuza wananchi katika mchakato wa
kuunda katiba ya nchi yao kama inavyofanyika sasa nchini mwetu, hili ni jambo
la hatari sana,” alionya Bashiru.
Bashiru anasema kuwa ili kuufanya mchakato wa sasa wa Katiba
mpya kuwa wa wananchi na kuepusha kuiingiza nchi kwenye machafuko na mauaji ya
wananchi wasio na hatia, mchakato wote unapaswa kurudiwa.
“Ili yasitufike yaliyotokea Kenya, tunapaswa kuanza upya
mchakato wa Katiba mpya, wananchi wapewe fursa ya kuumiliki mchakato mzima. Kwa
mfano, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kuchaguliwa na wananchi, si
kuteuliwa. CCM na wapinzani wanataka wajumbe wapatikane kwa kuteuliwa, mimi
nasema huo si utaratibu sahihi, dhana ya Bunge la Katiba inataka wajumbe wake
wapatikane kwa kuchaguliwa na wananchi, si kuteuliwa,” anabainisha Bashiru.
Ulivyopitishwa
Mjadala wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa iliyopita na
wabunge wengi wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni iliyosababisha Kiongozi wa
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
(CHADEMA) kutolewa nje na askari. Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa
upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa
upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment