Dar
es Salaam.
Watahiniwa
3,000 wa kujitegemea wako hatarini kutofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka
huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni Baraza la Mitihani la Taifa (Necta)
kutokuwa na taarifa zao za kulipia karo za mtihani huo pamoja na zile za
usajili.
Tayari
Necta imetuma barua kwa watahiniwa hao kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani mwaka huu.
Licha
ya maelezo hayo ya Necta, taarifa zinaonyesha kuwa watahiniwa hao walishalipa
ada za mtihani huo kupitia njia mbalimbali za kielektroniki zilizoainishwa na
baraza hilo, ikiwamo benki na kampuni za simu za mkononi.
Watahiniwa
walipaswa kulipa Sh35,000 ikiwa ni ada za mtihani huo kupitia wakala mbalimbali
walioteuliwa na Necta.
Gazeti
hili lilifanikiwa kuona barua ya Necta kwenda kwa mmoja wa wanafunzi
waliojisajili kufanya mtihani huo kwa mwaka 2013 ikimweleza kuwa, hataweza tena
kufanya mtihani huo kwa kuwa hakulipa karo ya mtihani huo.
Barua
hiyo ilieleza kuwa, kumbukumbu za Necta zinaonyesha kuwa wanafunzi hao
wamejiandikisha kufanya mtihani, lakini hawajawasilisha fomu za usajili wala
kulipa karo za mtihani huo.
“Hivyo
kwa barua hii, unafahamishwa kuwa umeondolewa kuwa mtahiniwa mwaka 2013,”
ilisema sehemu ya barua hiyo zilizosambazwa kwa watahiniwa hao.
Kutokana
na kuwepo hali hiyo, baadhi ya watahiniwa kutoka maeneo mbalimbali nchini,
wameanza kufuatilia Necta kujua hatima yao wakiwa na vielelezo vya malipo yao.
Ofisa
Habari wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alithibitisha kuwa
baraza hilo liliandika barua kwenda kwa watahiniwa takriban 3,000 waliokuwa
wamejiandikisha kama watahiniwa binafsi na kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani
huo kwa mwaka huu.
Alifafanua
kuwa, baadhi yao walifika Necta wakiwa na stakabadhi zilizothibitisha kuwa
wamelipa karo hiyo na hivyo kurudishwa kwenye kundi la watakaofanya mtihani huo
mwaka huu.
“Necta
hatupokei fedha moja kwa moja, tuna mawakala, kilichotokea ni kuwa baadhi ya
watu walilipa karo za mitihani, lakini kwenye mfumo wetu tulikuwa hatuoni kama
walilipa,” alisema na kuongeza:
“Kwa
hiyo watu wote walioandikiwa hizo barua ni wale ambao kwenye mfumo wetu
hawaonekani kama wamelipa, lakini wengi wa hawa walikuja na risiti zikionyesha kuwa
walikuwa wamelipa na wakarudishwa kwenye mfumo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment